ATCL yatangaza nauli zake

Na EPHRAHIM BAHEMU, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, January 17  2019 at  16:05

Kwa Muhtasari

Usafiri wa angani umekuwa ukitatiza nchini Tanzania kwa miezi ya hivi karibuni.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATCL) limetangaza gharama ya nauli kwa safari zake kati ya Dar es Salaam, Harare Zimbabwe na Lusaka Zambia zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kwa mujibu wa tangazo la shirika hilo lililotolewa jana Januari 16, nauli ya kwenda Lusaka (Umbali wa kilomita 1,936 kutoka Dar es Salaam) itakuwa Dola 218 za Marekani (TSh499,222) kwa safari moja na Dola 374 (TSh862,000) kwa safari ya kwenda na kurudi.

Safari ya kwenda jijini Harare ambalo lipo umbali wa kilomita zaidi ya 2,200 nauli yake ni Dola 214 (TSh493,000) kwa safari moja na Dola 317 (TSh855,000) kwenda na kurudi.

Pia, ATCL ambayo hivi sasa ina safari za kimataifa katika nchi tatu za Comoro, Burundi na Uganda ina ndege sita zinazofanya kazi, itakuwa ikifanya safari kati ya miji hiyo Jumanne, Ijumaa na Jumapili.

Ndege hizo za ATCL ni tatu aina ya Bombardier Q400-8; mbili aina ya Airbus A220-300 na moja Boeing 787-8 (Dreamliner).

Hata hivyo, ndege zake mbili aina ya Bombardier Q400-8 zinatarajiwa kufanyiwa matengenezo ya kawaida yajulikanayo kwa kitaalamu kama C Check hivi karibuni ambayo yatachukua hadi siku 21.

‘C Check’ kwa ndege hizo hufanyika pale ndege inapofikisha saa 4,000 ambazo imeruka angani.