http://www.swahilihub.com/image/view/-/4758788/medRes/2109313/-/xua584z/-/balozi.jpg

 

Bobi Wine ahoji juu ya kuteswa na kubambikiziwa kesi, balozi amkingia kifua Museveni

Mull Sebujja Katende (balozi) akiwa na Robert Kyagulanyi (Bobi Wine) na mwendeshaji wa kipindi  Shaka Ssali (kulia) wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha VOA (Straight Talk Africa) mjini Washington, Marekani  

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  10:00

Kwa Muhtasari

Adai Uganda ni nchi inayoheshimu mfumo wa demokrasia, sheria na haki za kibinadamu

 

Washington, Marekani. Mvutano baina ya balozi wa Uganda nchini Marekani, Mull Sebujja Katende na mbunge Robert Kyagulanyi ulijitokeza Jumatano, wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha VOA (Straight Talk Africa) mjini Washington, Marekani ambapo mbunge huyo alimhoji balozi ni kwa nini Serikali ya Uganda ‘inawatesa’ wananchi wake.

Wakati wa mahojiano hayo Kyagulani maarufu kama Bobi Wine katika madai yake aliishutumu Serikali ya Uganda kwa kuwatesa wananchi akionyesha yeye jinsi alivyoteswa baada ya kukamatwa na kikosi maalum cha kumlinda Rais Yoweri Museveni, huku kwa upande wake balozi Katende akisisitiza kuwa Uganda ni nchi inayoheshimu mfumo wa demokrasia, sheria na haki za kibinadamu.

Katika mahojiano hayo balozi Katende na Mbunge Kyagulanyi walitofautiana kuhusu hali ya siasa, haki na sheria nchini Uganda, mbele ya mwendeshaji wa kipindi hicho Shaka Ssali.

Bobi Wine yupo nchini Marekani kwa matibabu baada ya kupata majeraha akiwa mikononi mwa kikosi maalum cha jeshi kufuatia kukamatwa kwake huko Arua mwezi Agosti, 2018 na kuteswa.

Kwa upande wake Balozi amekanusha kuwa Uganda inaunga mkono mateso. Alisema chochote kilichomtokea wakati alipokamatwa, vyombo vya usalama, nchini Uganda vinafanya uchunguzi juu ya madai ya Bobi Wine.

Balozi Katende alisema kinachoendelea Uganda kwa wapinzani ambao wana maoni tofauti, ambao wameshindwa kuwashawishi wananchi kuwapa kura kuingia katika bunge, wanaishia kufikiria kuwa njia mbadala iliyo bora ni kusababisha fujo ili wapate ushindi kupitia machafuko ya kisiasa.

Aliongeza kuwa Bobi Wine hana haki ya kuzungumza kwa niaba ya raia wa Uganda kwa sababu anawakilisha jimbo moja tu, na kwamba aliye na haki ya kuzungumza kwa niaba ya taifa hilo ni Rais Yoweri Museveni.

Lakini Bobi Wine, alimkabili balozi Katende akidai kuwa Uganda inaongozwa kwa utawala wa kiimla, usiomruhusu mtu yeyote kumkosoa Rais Museveni.

Bobi Wine alitaka kujua kutoka kwa balozi ni kwa nini yeye akiwa mwananchi wa Uganda abambikiziwe kesi ya kumiliki bunduki mbili na risasi kadhaa, na baadaye mashtaka yafutwe katika mazingira tatanishi bila kueleza nani mmiliki wa bunduki hizo na bunduki zenyewe kutoweka.

Bobi Wine pia alikanusha madai ya Serikali ya Uganda kwamba yeye na wenzake wanatumiwa na nchi za nje.

“Nafanya kazi yangu kwa ajili ya nchi yangu Uganda. Nimezaliwa na kukuzwa katika mitaa duni nikiishi katika mabanda na Mungu amenisaidia kufika hapa nilipo kwenye studio za VOA kupitia msaada wa wananchi wenzangu,” alisisitiza Mwanasiasa huyo na kuongeza: “Nguvu hiyo ndio inayonifanya nizungumze kwa niaba ya raia wa Uganda bila woga wala upendeleo bila ya kujali anayeumizwa na ukweli wangu. Malengo yetu ni makubwa kuliko Muhozi, mtoto wa Museveni, hao wachache waliobahatika kuzaliwa katika maisha bora,” alisema.