Democrat washinda, wampania Trump

Kiongozi wa wachache katika Baraza la Wawakilishi, Nancy Pelosi akiwasalimia wafuasi wa chama cha Democratic baada ya kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa muhula wa katikati Jumanne. Kulia ni mwakilishi, Ben Ray Lujan. Picha na AFP  

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  09:25

Kwa Muhtasari

Ushindi waliopata Democrats una maana kuwa wataongoza kamati nyingi

 

Washington, Marekani. Chama cha Democratic Jumanne kilishindwa kumduwaza ‘mchawi’ Donald Trump katika uchaguzi wa katikati ya muhula, lakini rais huyo mwenye maneno mengi atakabiliwa na mkwamo baada ya wapinzani wake kudhibiti Bunge huku Republicans wakitawala Seneti.

Hatua ya Democrats kudhibiti Bunge ina maana kwamba wataongoza kamati nyingi za Bunge ambazo sasa zitatumika kuanzisha uchunguzi dhidi ya Trump, ikiwa ni pamoja na kuhoji rekodi zake za ulipaji kodi ambazo alikataa kuzionyesha wakati wa kampeni mwaka 2016.

Wademocrat wanasema kuwa watamfundisha Trump kwamba hayuko juu ya sheria.

Wakichochewa na hali isiyo ya kawaida ya watawala wanaojinasibu kwa uzalendo na watu wa mijini na vijijini kutoridhishwa na Rais Trump, Democrats walifanikiwa kushinda na kudhibiti Bunge kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2011.

Chama hicho kilikuwa kinatarajiwa kupata viti zaidi kuliko mwaka wa 2006, mwaka ambao walitoa kile rais wa wakati huo George W. Bush alielezea kuwa “anguko.”

“Nawashukuru, tuliwazidi,” alisema kiongozi wa waliowachache katika bungeni Nancy Pelosi – ambaye anatarajiwa kuwa Spika wa baadaye. “Shukrani, kesho itakuwa siku mpya kwa Marekani.”

Aidha, Nancy alisema chama kitaweka utaratibu wa Kikatiba wa kutathmini na kumdhibiti Trump.

Matokeo yaliyotolewa Jumatano asubuhi yameonyesha kuwa Democrats walinyakua viti 222 vya bunge, hivyo kuwa juu kidogo ya viti 218 vinavyohitajika kuwa na wabunge wengi lakini wakipata mshtuko kukosa viti 23.

Republican watamba

Lakini ilikuwa hadithi nyingine upande wa Seneti ambako Chama cha Republican cha Rais Trump kilitarajiwa kujikusanyia viti 54 dhidi ya 42 vya Democrats ilhali viti 51 ndivyo vinahitajika kuwa na wingi mkubwa. Hadi asubuhi Republican walikuwa wamenyakua viti 51 dhidi ya 45.

Trump aliuita usiku wa Jumanne kuwa ‘mafanikio makubwa’ kupitia Twitter na alijisifu kwa ‘uchawi’, lakini ukweli ni kwamba Wademocrat sasa watatumia wingi wao bungeni kuzuia ajenda zake katika kipindi cha miaka miwili iliyosalia.