http://www.swahilihub.com/image/view/-/4755492/medRes/2107136/-/84vehez/-/uno.jpg

 

Lula ajiuzulu ugombea urais Brazil, Fernando Haddad kuipeperusha bendera

Fernando Haddad,

Picha ya Desemba 1, 2016, ya Fernando Haddad, akiwa meya wa Sao Paulo, alipokuwa katika kongamano la 'Mayors C40 Summit 2016' jijini Mexico City, Mexico. Haddad anachukua nafasi ya rais wa zamani Luiz Inacio Lula da Silva aliyelazimika kujiuzulu ugombea Septemba 11, 2018, kuendelea kutumikia kifungo. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA na PETER MBURU

Imepakiwa - Wednesday, September 12  2018 at  09:51

Kwa Muhtasari

Aliyekuwa meya wa Saulo Paulo, Fernando Haddad sasa ndiye mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha wafanyakazi Brazil (PT) katika uchaguzi wa Oktoba akichukua nafasi ya Rais wa zamani Luiz Inacio Lula da Silva anayetumikia kifungo jela.

 

RIO DE JANEIRO, Brazil

ALIYEKUWA meya wa Saulo Paulo, Fernando Haddad sasa ndiye mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha wafanyakazi Brazil (PT) katika uchaguzi wa Oktoba akichukua nafasi ya Rais wa zamani Luiz Inacio Lula da Silva anayetumikia kifungo jela.

Hii ni kufuatia tangazo la Jumatatu lililofanywa katika hafla ya umma kando na jela ya Kusini mwa jiji la Curitiba, ambapo Lila anahudumia kifungo cha miaka 12 kwa kesi ya ufisadi.

“Leo tunamleta Fernando Haddad kuwa mgombeaji wa urais wetu,” akasema Rais wa chama cha PT Gleisi Hoffman.

Katika barua iliyosomwa kwenye mkutano huo, Lula alisema anaunga mkono kuteuliwa kwa Haddad kuwa mgombea urais, ambaye alikuwa akigombea pamoja naye kama “naibu wa rais ambaye alikuwa mwaminifu.”

“Ninataka kuwaomba wote ambao walinipigia kura kumuunga mkono rafiki yangu Fernando Haddad kuwa rais wan chi kutoka rohoni,” akaongeza Lula.

Haddad alisema kuwa kama Wabrazili wengi pia naye alikuwa na huzuni kuwa Lula hatakuwa Rais wao tena.

Jumanne ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa PT kumteua mtu wa kuchukua nafasi ya Lula, huku Manuela d’Avila akiteuliwa kuwa naibu mgombeaji wa Haddad.

Mahakama kuu ya uchaguzi Brazil ilimfungia Lula kugombea kiti cha urais kwenye uchaguzi wa Oktoba 7 kutokana na rekodi yake mbaya ya makosa ya jinai. Mawakili wake bado wana rufaa moja ambayo haijaamuliwa kuhusiana na kupigwa kwake marufuku kugombea.

Kulingana na kura za maoni, Lula alikuwa mbele ya wagombeaji wengine 13 kwa mbali, akiwa na uungwaji mkono wa takriban asilimia 40, huku Haddad akiwa na asilimia tisa pekee ya uungwaji mkono katika kura ya maoni iliyochapishwa Jumatatu.

Kura ya utafiti

Anayeongoza kulingana na matokeo ya kura hiyo ya maoni sasa ni aliyekuwa mkuu wa jeshi Jair Bolsonaro ambaye alipata asilimia 24, na ambaye alijeruhiwa vibaya na kisu wakati wa hafla ya kisiasa wiki iliyopita.

Bado anaendelea kutibiwa huku familia yake ikisema ataendeleza kampeni zake kwenye mitandao ya kijamii anapoendelea kupata nafuu, japo hospitali alipo imesema hali yake ya afya iko shwari.

Lula alifungwa Aprili baada ya kupatikana na hatia iliyohusiana na viusa vya ufisadi. Mzee huyo wa miaka 72, hata hivyo amepokea sifa tele kwa kuinua hali ya uchumi ya Brazil, kumaliza umasikini na kuinua hadhi ya Brazil alipokuwa uongozini kati ya 2003 na 2010.

Lakini chama chake kimetaja kesi zinazoendela kortini dhidi ya rais huyo wa zamani kuwa mbinu ya kumfungia kutowania urais tena, kwani amepigana kwa muda mrefu aruhusiwe kugombea.