http://www.swahilihub.com/image/view/-/3406064/medRes/1168738/-/3t9je1/-/MagufuliRais.jpg

 

IMF yaionya Tanzania dhidi ya kubana matumizi

Rais John Magufuli akitoa hotuba

Rais John Magufuli akihutubu awali. Picha/AFP 

Na JULIUS MNGANGA

Imepakiwa - Wednesday, January 11  2017 at  14:43

Kwa Mukhtasari

Dar es Salaam, TANZANIA

Licha ya kukua kwa uchumi, Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeionya Tanzania dhidi ya  sera zake za kubana matumizi na matamko kuhusu wafanyabiashara.

 

Pamoja na kusifu hatua za kumarisha mapato ya Serikali, mkutano wa Bodi ya Wakurugenzi wa IMF  uliofanyika Januari 9,2017 ambao ulifanya mapitio ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania, umeonya masuala kadhaa ambayo yatakuwa changamoto endapo hayatashughulikiwa kwa wakati.

Ripoti hiyo ya IMF kuhusu Tanzania inaeleza kuwa uchumi unaendelea kuwa imara baada ya kutoyumba katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 na kwamba utaendelea kukua kwa asilimia 7 kama ulivyopangwa.

Pia ripoti hiyo iliyowekwa kwenye mtandao wa IMF inasema mfumuko wa bei ulishuka hadi asilimia 5 kiwango ambacho ni tofauti na matarajio ya Serikali wakati nakisi katika akaunti ya madeni ya nje imeonekana  kuwa ndogo kwa kuwa kulikuwa na uagizaji mdogo wa bidhaa kutoka nje.

“Pamoja na yote hayo kuna athari ambazo zinaweza kuathiri  kukua kwa uchumi zikitokana na msimamo mkali wa sasa katika sera za kukuza uchumi, kasi ndogo ya kukua kwa ukopaji ambayo inaweza kusababisha kuchukua muda mrefu,”

inasema taarifa hiyo ya IFM ambayo ni chombo cha kimataifa kinachosaidia ukuaji wa uchumi wa nchi wanachama kwa  kuzitengenezea  mikakati na kuzikopesha fedha.

Taarifa hiyo pia inasema mambo mengine ni kasi ndogo ya utekelezaji wa uwekezaji kwa umma na hali ya kutokuwa na uhakika sekta binafsi kuhusu mikakati mipya ya kiuchumi ya Serikali.

Ripoti hiyo inaongeza,”Mamlaka zinatakiwa zilegeze masharti na kuzidisha juhudi za kusimamia uchumi wake ili kupata mafanikio yanayotarajiwa  ndani ya muda wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa.”

Kufuta safari za nje

Hatua kadhaa zimechukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kubana matumizi zikiwamo kufuta safari za nje kwa watumishi wa umma, kuzuia mikutano ya idara na taasisi za umma hotelini, kufuta sherehe za kitaifa na kuhamisha akaunti za taasisi za umma  kutoka benki za biashara na kwenda Benki Kuu.

Serikali pia imeagiza taasisi zake kutotumia benki za biashara kuhifadhi  fedha zake na badala yake makusanyo yote yaende Benki Kuu jambo linalolalamikiwa kuwa limesababisha fedha kupotea kwenye mzunguko.

Akitoa tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu kuanzia  Juni hadi Disemba 2016, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

“Lengo ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji  na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya maendeleo,” alisema Waziri Mpango.

Licha ya Serikali  kueleza kwamba amana za wateja  wenye benki za biashara zilipungua kidogo kutokana na uamuzi wa kuhamishia fedha za taasisi na idara zake Benki Kuu, shirika hilo la fedha limeonya kuhusu kupungua kwa mkopo kutoka taasisi za fedha na benki za biashara.

Amana zimepungua

Dk Mpango alieleza kuwa amana za wateja kwenye benki za biashara  zimepungua kutoka Sh20.73trilioni Disemba 2015 mpaka 20.57 Septema 2016. Amana za Serikali  kwenye benki hizo ni asilimia tatu tu ya amana zote.

Pamoja na hayo yote, benki nyingi zimepunguza kiasi cha mikopo zilizokuwa zinatoa kwa wafanyabiashara, jambo  ambalo IFM imeona si zuri kwa uchumi wa Tanzania ingawa Dk Mpango ana maoni tofauti.

Alisema,” Kupungua kwa mikopo kwa sekta binafsi katika miezi ya hivi karibuni  siyo kwa Tanzania pekee. Ukuaji huo umepungua kutoka asilimia 19.7 hadi asilimia 4.1 nchini Kenya wakati Uganda ilitoka asilimia 25 mpaka asilimia -1”

Kutokana na sababu zisizofahamika, Serikali  inatambua kufungwa kwa takriban biashara 2,000 kati ya Agosti na Oktoba mwaka jana kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.

Hii ni mara ya pili kwa shirika hili kuionya Tanzania kuhusu sera zake  za kiuchumi. Julai mwaka jana, IFM ilionya kuhusu shauku ya kutekeleza miradi mikubwa kama vile ujenzi wa bandari, barabara na reli kwa kutumia fedha za mikopo  bila kuzingatia uwezo wa kulipa.

Mikopo mikubwa

Licha ya kumpongeza Rais Magufuli kwa hatua zake za kupambana na rushwa na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara, IMF imeonya kuhusu mikopo mikubwa ambayo Serikali inachukua kwa ajili ya miradi yake.

Kwa mfano kupokea dola 7.6 za Marekani kutoka Serikali ya China kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati yenye urefu wa  kilomita 2,200.

Hoja nyingine ni  sekta binafsi  kutokuwa na uhakika wa kiuchumi ya Serikali licha ya kuimarika kwa akiba ya fedha za kigeni ambayo ni dola 4.05 bilioni ambazo zinatosha kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi 4.1.

“Vita dhidi ya rushwa zimeimarisha  mapato, ushirikishwaji wa wadau wote hasa sekta binafsi kufanikisha sera zilizopo ni jambo muhimu sana,” inasema IFM.

Akizungumzia suala hilo, Profea Gaidence  Mpangala wa Chuo Kikuu cha Iringa alisema  si IFM pekee  iliyoiona suala hilo bali hata wasomi. Alisema kuporomoka kwa uchumi  kunasababishwa na sera za kubana  matumizi ambayo imeibuliwa bila kufanya utafiti.

“Ikumbukwe kwamba awali nchi yetu ilikuwa ya kijamaa, ilimiliiki  uchumi wake. Baadaye sekta binafsi iliruhusiwa  kuendesha uchumi  na hizi sekta zilishirikana na Serikali  ambayo ndiyo yenye fedha,” alisema. Alisema kwa sasa sekta binafsi inakosa kipato kwa sababu mshirika wake mkuu ambaye ni serikali amebana matumizi.

Zimeporomoka

“Hoteli, nyumba za kupanga, magari na wazabuni wengi  walitegemea watumishi wa serikali yenyewe ili kupata kipato lakini sasa hizi zimeporomoka kwa sababu Serikali inabana matumizi .

Zamani  hayo wanayobana ndiyo yalifanya uchumi ustawi  na mzunguko wa fedha ulikuwapo, alisema Profesa Idris Kikula wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Alisema  kusuasua kwa uchumi  kumekuja baada ya Rais John Magufuli  kuanza kushughulika na rushwa, watumishi hewa, wanafunzi hewa na matumizi mabaya ya madaraka.

Alisisitiza kuwa hatua zote hizi alizochukua Magufuli ni lazima mzumguko wa fedha utaathirika kwani ile mianya yote  iliyotumika kujipatia fedha  isivyo halali imezibwa.

“Mbona hawasemi Rais alivyozuia uingizwaji wa makontena yasiyolipiwa kodi bandarini, Escrow na matumizi mabaya ya fedha badala yake wanainyooshea vidole Serikali?” aliuliza.