Jaji Weber apinga ombi la Roraima

Jaji wa Mahakama ya Juu nchini Brazil, Rosa Weber  

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  08:52

Kwa Muhtasari

Limekiuki Katiba ya Shirikisho na mamlaka ya majimbo, manispaa

 

Rio de Janeiro, Brazil. Jaji wa Mahakama ya Juu, Rosa Weber amekataa ombi lililowasilishwa juzi na Serikali ya Jimbo la Roraima la nchi hiyo kufunga mpaka wake na Venezuela.

Uamuzi huo ulitolewa saa chache baada ya jaji wa Mahakama ya Shirikisho kuamua kwamba Serikali ya eneo hilo inaweza kuzuia uingiaji wa raia wa Venezuela wanaoomba hifadhi ya ukimbizi Brazil.

“Hiyo haihalalishi kwa sababu tu ya matatizo ambayo kimsingi hutokana na malazi ya wakimbizi, ukaanza na suluhisho jepesi la kufunga milango ambalo kimtazamo ni sawa na ‘kufunga macho’ na ‘kukunja mikono,” alisema Jaji Weber katika uamuzi wake.

Kwa mujibu wa jaji huyo, zaidi ya kutokuwapo mazingira ya kisheria kuruhusu kuweka zuio hilo, ombi la Serikali ya Roraima pia linakwenda kinyume na “msingi wa Katiba ya Shirikisho, Sheria za Brazil na mikataba iliyoridhiwa na Brazil.”

Jaji wa Shirikisho katika Jimbo la Roraima, Helder Girao Barreto alihalalisha uamuzi wake kwa kusema ni jambo la lazima kukataa wazo kwamba, katika masuala yanayohusu uhamiaji, muungano unaweza kufanya kila kitu, na majimbo na manispaa lazima yabebe kila kitu. Aliongeza kwamba Brazil inaweza “kuridhia sera ya uhamiaji ambayo inatambua suala hilo ilimradi tu haikiuki Katiba ya Shirikisho na mamlaka ya majimbo pamoja na manispaa.