Joka la futi tano lapatikana chooni

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Wednesday, January 11  2017 at  14:16

Kwa Mukhtasari

VIRGINIA, AMERIKA

JOKA la rangi ya manjano lenye urefu wa futi tano lilipatikana ndani ya tundu la choo, kulingana na maafisa wa kuhifadhi wanyama.

 

Maafisa hao walisema kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa joka hilo la ‘anaconda’ lilipatikana na mtu aliyekuwa ameenda kujisaidia.

“Sote tulishtuka. Tulitarajia pengine tuliitiwa nyoka mdogo wa mwituni lakini kwa mshangao wetu, tukapata ni anaconda wa rangi ya manjano,” taarifa yao ilisema.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa joka hilo huweza kukua hadi kwa urefu wa futi 13 na uzito wa zaidi ya kilo 45.

“Ingawa hawana sumu, huwa wanaweza kuwa wenye hatari wanapokomaa hasa wasipozoea kuishi na binadamu,” wakasema, huku wakishuku joka hilo lilikuwa limefugwa nyumbani likatoroka.

Waliomba wanaofuga nyoka nyumbani wawe waangalifu zaidi na wahakikishe wana uwezo wa kuwatunza kabla kufuga.

Walifanikiwa kuliondoa kisha wakamtafutia makao mema, na aliyemchukua akampa jina la ‘Sir Hiss’.

Mkuu wa idara ya kudhibiti wanyama katika eneo la Arlington Bi Jennifer Toussaint alinukuliwa kusema: “Huenda kulikuwa na joto jingi ndipo joka likaamua kuingia majini. Wao huweza kuingia mahali popote palipo na shimo kirahisi sana.”

 

Imekusanywa na VALENTINE OBARA