Magufuli na Museveni wakejeli ICC kupelelza Burundi

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Sunday, November 12  2017 at  16:51

Kwa Muhtasari

RAIS wa Tanzania, John Magufuli, na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni, walikashifu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa kufungua upelelezi dhidi ya madai ya uhalifu wa kivita Burundi.

 

Taarifa kutoka kwa afisi ya rais wa Tanzania ilisema viongozi hao wawili walikashifu hatua hiyo walipokutana magharibi mwa Uganda.

“Rais Magufuli alisema uamuzi huo umevuruga juhudi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo ilibuni kamati yenye jukumu la kutafuta suluhisho kuhusu vita vya Burundi,” ikasema taarifa hiyo.

Kamati yenyewe inasimamiwa na Rais Museveni akisaidiana na aliyekuwa rais wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Rais Museveni ndiye kiongozi wa sasa wa EAC inayojumuisha Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Kwa upande wake, Rais Museveni alikashifu ICC kwa “kuingilia vibaya juhudi za EAC”. Alhamisi iliyopita, ICC ilifichua kuwa majaji wake waliruhusu upande wa mashtaka uendeleze upelelezi kuhusu madai ya uhalifu wa kivita ambao ulitokea Burundi kati ya Aprili 26, 2015 hadi Oktoba 26, 2017.