http://www.swahilihub.com/image/view/-/4803372/medRes/2135699/-/yg759f/-/aribe.jpg

 

Mahakama sasa ipo huru kushughulika na Maribe

Mtangazaji wa Citizen TV, Jacque Maribe  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  17:06

Kwa Muhtasari

Wakili wake athibitisha hana matatizo yoyote ya kiakili

 

Nairobi, Kenya. Mtangazaji Jacque Maribe anayeandamwa na tuhuma za mauaji ya msichana Monica Nyawira Kimani hana matatizo yoyote ya kiakili, amesema wakili wake Katwa Kigeni.

Vyombo vya habari Ijumaa viliarifiwa kwamba Maribe alifanyiwa uchunguzi wa kiakili jana katika Hospitali ya Mathari iliyoko jijini Nairobi, inayoshughulikia wenye shida za kiakili na ikabainika hana matatizo yoyote.

Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Jaji Jumatatu aliagiza mtangazaji huyu na mchumba wake Joseph Irungu, maarufu Jowie, ambaye pia ni mshukiwa mkuu wa mauaji ya Monica kufikishwa katika mahakama kuu ili kufunguliwa mashtaka.

Haji alisema ana ushahidi wa kutosha kushtaki wawili hao kwa mauaji. Ombi la washukiwa hao kutaka kuachiliwa kwa dhamana liligonga mwamba, ambapo Jaji Jessie Lessiet aliamuru warejeshwe rumande na Maribe achunguzwe kiakili.

Juhudi za wakili Katwa Kigeni kujaribu kushawishi korti imsomee Maribe mashtaka kabla ya kukaguliwa kiakili, ziligonga mwamba. Pia Jaji Lessiet aliagiza mchumba wa mtangazaji huyu apelekwe hospitalini kutibiwa jeraha la risasi aliyojipiga.

Upande wa mashtaka uliwaambia korti kuwa Irungu alishafanyiwa uchunguzi wa kiakili, na kuonekana kwamba ni timamu kusomewa mashtaka na kufunguliwa kesi.

Kwa kawaida, kesi za uhalifu zinazohusiana na mauaji korti huagiza washukiwa kufanyiwa uchunguzi wa kiakili ili kuona iwapo wana akili timamu, kabla ya kusomewa mashtaka na kufunguliwa kesi.

Lessiet alisema wawili hao watarejea kortini mnamo Jumatatu, Oktoba 15 ili kusomewa mashtaka yao. Irungu amekuwa kizuizini tangu Septemba 25 huku Maribe Septemba 30.

Monica 28, alipatikana ameuawa mnamo Septemba 20, 2018 kwenye nyumba yake katika mtaa wa kifahari wa Kilimani, jijini Nairobi. Marehemu alizikwa nyumbani kwao Gilgil, kaunti ya Nakuru.

Aidha, alikuwa mfanyabiashara Juba, Sudan Kusini na kabla ya kukumbana na mauti alikuwa amerejea Kenya akitarajiwa kusafiri Dubai kwa likizo.

Jirani ya Irungu na Maribe katika nyumba yao Lang'ata, Brian Kassaine, ambaye pia ni mojawapo wa washukiwa jana aliachiliwa na korti Kiambu, duru zikiarifu kwamba atakuwa shahidi wa upande wa mashtaka. Bunduki ya Kassaine inatuhumiwa kuwa ndiyo ilitumiwa na Irungu kumuua Monica na kujipiga risasi.

Inasemekana awali mshukiwa huyo alikuwa ametoa taarifa ya kudanganya akizuia washukiwa wakuu, lakini aliahidi kwamba atakuwa shahidi wa mauaji hayo.