http://www.swahilihub.com/image/view/-/4800842/medRes/2136249/-/7q3jfpz/-/jamal.jpg

 

Majasusi waliomuua mwanahabari wafichuliwa na magazeti

Aliyekuwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi  

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  09:10

Kwa Muhtasari

Watuhumiwa hao wanasakwa na mamlaka za Uturuki kwa mahojiano

 

 

Ankara, Uturuki. Gazeti la Sabah lenye mafungamano na Serikali ya Uturuki limetaja majina na kuchapisha picha za kikosi cha majasusi 15 wanaodaiwa kuhusika katika kisa cha kupotea mwandishi wa habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi.

Habari kama hizo zimeandikwa pia na gazeti la New York Times la Marekani

Kwa mujibu wa gazeti hilo, watu hao kutoka Saudi Arabia walisafiri hadi Istanbul siku ambayo Khashoggi alitoweka.

Gazeti hilo limedai watu hao waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Ataturk, Istanbul, Oktoba 2 na uchunguzi wake unaonyesha watu 12 kati yao waliwasili asubuhi ya siku hiyo, kulingana na picha zilizochapishwa ambazo zimepatikana katika ofisi ya ukaguzi wa pasipoti za kusafiria.

Pia, gazeti la Sabah linadai watu hao 15 waliondoka katika muda tofauti. Hata hivyo, gazeti hilo halijaeleza jinsi lilivyozipata picha pamoja na data hizo.

Awali duru za kiusalama zililiambia Shirika la Habari la Reuters kwamba raia 15 wa Saudia, wakiwemo maofisa, waliwasili Istanbul na kuingia kwenye ubalozi wao mdogo Oktoba 2 na kisha waliondoka nchini humo. Watuhumiwa hao wanasakwa na mamlaka za Uturuki kwa mahojiano.

New York Times lafichua

Katika hatua nyingine gazeti la New York Times la Marekani limefichua kwamba viongozi waandamizi wa Saudi Arabia waliandaa kikosi cha mauaji cha watu hao kumvizia na kumkamata mwandishi wa habari mkosoaji Jamal Khashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo uliopo Istanbul.

Miongoni mwa watu waliokuwemo kwenye timu hiyo ya mauaji ni mtaalamu wa utambuzi wa uhalifu ambaye alibeba msumeno kwa lengo la kumkatakata vipande vipande Khashoggi baada ya kumuua gazeti hilo liliandika Jumanne, likimnukuu ofisa wa Marekani ambaye hakutajwa jina lake.

Kikosi hicho cha mauaji kilikamilisha operesheni ya mauaji katika muda wa saa mbili na kiliondoka Uturuki kwenda nchi mbalimbali, chanzo hicho kililiambia gazeti hilo kikinukuu taarifa kutoka “maofisa wa ngazi ya juu wa Uturuki”.

“Ni mithili ya kisa cha kubuni,” ofisa wa ngazi ya juu wa Marekani alinukuliwa akisema akirejea filamu za ghasia za Hollwood zilizoandaliwa na Mkurugenzi Quentin Tarantino kwa michoro sanifu mwaka 1994.

Shutuma kwamba utawala wa Saudi Arabia uliamuru mauaji dhidi ya Khashoggi yatazidisha shinikizo kutoka Marekani na washirika wake wanaotaka kuona uchunguzi wa wazi jambo linaloweza kuathiri uhusiano baina ya mataifa hayo ikiwa halitazaa matunda. Maofisa wa Saudi Arabia wamekana kuhusika juu ya kutoweka kwa Khashoggi na mauaji yanayodaiwa, wakisema aliondoka kwenye ubalozi huo mdogo Oktoba 2. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameitaka Saudi Arabia kuthibitisha mwandishi huyo alivyotoka nje ya majengo.