http://www.swahilihub.com/image/view/-/4660546/medRes/2043041/-/11smrb3/-/trump.png

 

Marekani yachoka kuibeba NATO

Rais wa Marekani, Donald Trump  

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, July 13  2018 at  09:40

Kwa Muhtasari

Jumuiya zitenge asilimia nne ya pato katika bajeti ya ulinzi

 

Brussels, Ubelgiji. Rais Donald Trump wa Marekni ametishia kuiondoa nchi yake katika Jumuiya ya Kujihami (NATO) ikiwa nchi za Ulaya hususani Ujerumani, Ubelgiji na Hispania hazitoongeza bajeti zao za ulinzi.

Tishio hilo ni mwendelezo wa kauli za kiongozi huyo dhidi ya washirika wanaounda jumuiya ya NATO, akisema marais wengi wa Marekani walikuwa wakijaribu bila mafanikio kwa miaka mingi kuilazimisha Ujerumani na nchi nyingine tajiri za NATO kuongeza bajeti za ulinzi dhidi ya Urusi na hivyo kuiacha Marekani pekee ikilipa mabilioni ya dola kwa ajili ya ulinzi.

Rais Trump amezitaka nchi tajiri zilizoko katika jumuiya hiyo zitenge asilimia nne ya pato jumla la nchi zao katika bajeti ya ulinzi, akidai kwamba Marekani inatumia mabilioni ya dola kutoa ruzuku Ulaya. Trump amechukua msimamo huo unaotajwa kuwa wa kibabe katika mkutano wa NATO mjini Brussels, Ubelgiji akihoji thamani ya muungano huo ambao umekuwa ukiielekeza sera ya nje ya Marekani kwa miongo kadhaa.

Trump pia alikabiliwa vilivyo na nchi za Ulaya kwa kumkumbatia Rais Vladmir Putin wa Urusi lakini akaigeuzia kibao Ujerumani akimulika uhusiano wa nchi hiyo ya Urusi na kudai kwamba serikali ya Kansela Angela Merkel imejiachia na kudhibitiwa kikamilifu na kutekwa nyara na Urusi kutokana na maslahi ya kutaka bomba la gesi asilia kutoka Urusi.

Amedai Ujerumani imeanza kuilipa Urusi mabilioni ya fedha kwa ajili ya mahitaji yao ya nishati kutoka bomba la Urusi, na hilo ni jambo lisilokubalika.

Wakosoaji wanahisi msururu wa kauli mpya za Trump na hasa za kulazimisha nchi za Ulaya ziongeze kiwango cha bajeti ya ulinzi zinatishia kuhujumu muungano huo wa miongo kadhaa ulioanzishwa kwa lengo la kukabiliana na uchokozi wa uliokuwa Muungano wa Sovieti.

Kansela Merkel ambaye binafsi alilelewea katika Ujerumani Mashariki ya kikomunisti amezungumzia jinsi alivyowahi kushuhudia hali ya kudhibitiwa na muungano wa Usovieti na kwamba anafurahi wakati huu kwamba kuna mshikamano katika uhuru kama Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani.

Amesisitiza juu ya mshikamano wa jumuiya ya NATO katika kuamua sera zao. Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May pia ametowa wito wa mshikamano miongoni mwa washirika wa NATO akitaja kwamba wakati Urusi inashirikishwa lazima suala hilo lifanyike chini ya msimamo mmoja wa mshikamano na udhabiti katika NATO.