http://www.swahilihub.com/image/view/-/4027830/medRes/1709313/-/ohteauz/-/maduro.jpg

 

Marekani yadhamiria kumng’oa Maduro

Nicolas Maduro

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela aendesha gari wakati wa mgomo ulioitishwa na upinzani Julai 20, 2017. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  11:12

Kwa Muhtasari

Kwa sasa kiongozi wa upinzani nchini Venezuela, Juan Guaido anachunguzwa na serikali baada ya kujitangaza 'Rais wa muda wa mpwito'.

 

CARACAS, Marekani

MAREKANI imeiwekea vikwazo vya kiuchumi Venezuela kwa lengo la kuona Serikali yake inakosa nguvu ya kujiendesha huku ikimuunga mkono mpinzani aliyejitangaza kuwa kiongozi wa mpito.

Takriban mataifa 20 yakiwamo yenye nguvu ya kiuchumi na ushawishi mkubwa katika siasa duniani, zimeweka wazi msimamo wa kumtaka Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro kuondoka madarakani.

Marekani, Uingereza na Ufaransa, ni miongoni mwa mataifa yanayoshinikiza Maduro kuachia madaraka kwa amani huku zikimuunga mkono mpinzani aliyejitangaza kuwa kiongozi wa mpito wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta, Juan Guaido.

Tayari Marekani imeshatangaza hatua mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha Maduro aliyeanza muhula mpya wa kuiongoza nchi hiyo mwaka jana, ikiwamo kuiwekea vikwa Kampuni ya Mafuta ya Venezuela (PDVSA).

Imepiga marufuku kwa raia wake kufanya shughuli yoyote ya kifedha na kampuni hiyo kuonyesha ni kwa jinsi gani haikubaliani na utawala wa Maduro.

Aidha, imeliomba jeshi la nchi hiyo kukubali mabadiliko na kuipitisha nchi salama katika kipindi cha mpito, kutomuunga mkono Maduro na kuungana na Guaido katika mabadiliko hayo.

Vikwazo dhidi ya kampuni hiyo ambayo ni miongoni mwa kampuni zinazouza mafuta kwa wingi katika soko la Marekani, vinalenga kuiondolea nguvu ya kiuchumi Serikali ya Maduro.

Hatua hiyo mbali na kutikisa uchumi wa Venezuela, pia inaweza kuwaondolea washirika wa karibu wa Maduro ushawishi wa kuendelea kumuunga mkono hatua ambayo inaweza kumpunguzia nguvu ya kushikilia madaraka.

Trump aonya

Mara baada ya Guaido kujitangaza kuwa kiongozi wa mpito wa Venezuela, Rais Donald Trum alisema nchi yake inamuunga mkono.

Trump aliionya Venezuela kwa hatua yoyote itakayochukua kukandamiza raia au wanasiasa wa upinzania na kusema itatumia njia mwafaka kulinda na kusimamia haki zao.

Mtihani kwa Maduro

Tangu kuanza kwa wimbi la kumtaka aondoke madarakani, Maduro amezungumza mara kadhaa na mara zote amekuwa akiilalamikia Marekani kutaka kuitawala nchi yake kupitia wanasiasa aliowaita ni vibaraka.

Anasema hayuko tayari kuona hilo likitimia na kuapa kwamba ataendelea kuilinda nchi yake katika kila hali ili rasilimali zilizopo ziendelee kuwanufaisha Wavenezuela.

Hata hivyo, kinachotokea sasa kinaonekana kuwa mtihani mzito kwa Maduro kwani ni tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo ingawa hapakuwa na uhusiano mzuri kati ya Marekani na nchi yake, lakini mwitikio wa mataifa mengi yakiwamo yenye nguvu kuungana na Marekani kunatoa ishara mbaya zaidi.

Maduro aliijibu Marekani kwa kutoa saa 72 kwa wanadiplomasia wa nchi hiyo kuondoka nchini humo na kutangaza kuvunja uhusiano. Hata hivyo, Marekani ilisema Maduro kwa sasa hana mamlaka ya kutoa amri hiyo.

Mustakbali wa taifa hilo unaelezwa kuwa mikononi mwa jeshi ambalo mpaka sasa linaendelea kumuunga mkono Maduro ingawa inadaiwa ni viongozi wa vyeo vya juu ndio wanaomtii zaidi ili kutetea maslahi yao huku wapiganaji wa chini wakionekana kuwa tayari

kubadilika wakati wowote.

 

 

 EU, Urusi waunga mkono

Tofauti na mataifa mengine ya Magharibi, Urusi imehamasisha mshikamano kwa Maduro hatua inayoungwa mkono na Cuba, Uturuki na China.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, anasema kinachoendelea Venezuela kinakiuka sheria za kimataifa zinazotaka kuheshimiwa kwa mambo ya ndani ya nchi.

Baadaye Rais Jair Bolsonaro wa Brazil alisema: “Brazil inamtambua Juan Guaido kuwa kiongozi wa mpito wa Venezuela.”

Aliongeza. “Brazil itamuunga mkono kisiasa na kiuchumi ikiwa ni hatua ya kuirudisha nchi hiyo katika utawala wa kidemokrasia na amani ya jamii”.

Kwa upande wa Rais wa Baraza la Jumuia ya Ulaya (EU), Donald Tusk, alituma ujumbe kupitia akaunti yake ya tweeter akisema. “Naamini nchi za Ulaya zitaunga mkono demokrasia nchini Venezuela”.

Aliongeza: “Tofauti na Maduro, Bunge likiongozwa na Guaido linayo mamlaka ya kidemokrasia kwa watu wa Wavenezuela”.

Mbali na Brazil, Colombia, Chile, Peru, Ecuador, Argentina, Paraguay na Canada zimeungana na Marekani kumtambua Guaido huku China, Iran, Uturuki, Mexico, Bolivia na Cuba zikisema zinaendelea kumtambua Maduro kuwa kiongozi halali wa Venezuela. Shirikisho la Nchi za Amerika (OAS), nalo limetangaza kumtambua kiongozi huyo wa mpito.

Mwaka 2017, Venezuela ilitishia kujiondoa katika shirikisho hilo likilituhumu kuingilia mambo yake ya ndani.

Guaido ni nani?

Umaarufu na kusikika kwake kulipata nguvu baada ya kuwa kiongozi wa Bunge la Taifa ambalo linatawaliwa na upinzani kutokana na idadi kubwa ya wabunge wake.

Alipokuwa mwanafunzi, aliongoza maandamano dhidi ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Hugo Chavez ambaye wakati wa uhai wake alimchagua Maduro kuwa mrithi wa kiti cha urais.

Kuchaguliwa kwake kuwa kiongozi wa Bunge hilo kuliuzindua upinzani ambao katika miaka ya karibuni ulionekana kupoteza nguvu.

Akijitangaza kuwa kiongozi wa mpito, alisema kwa nafasi yake anachukua uongozi wa nchi hiyo kwa muda hadi hapo uchaguzi mpya utakapoitishwa.

Maduro aliyeingia madarakani mwaka 2013 baada ya kufariki Chavez, amekuwa akikabiliwa na shutuma mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi hiyo huku kubwa likiwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Uhaba wa bidhaa na huduma muhimu yakiwamo matibabu na chakula umeendelea kuitesa nchi hiyo ambapo inakadiriwa Wavenezuela milioni tatu wameondoka nchini humo na kukimbilia ughaibuni.

Hata hivyo, bado kuna maelfu ya wananchi wanaoendelea kuiunga mkono Serikali wakiamini changamoto zilizopo ni mkakati uliotengenezwa na mataifa ya nje na kuwatumia viongozi wa upinzani kuidhoofisha nchi yao.

Kinachochochea machafuko

Miongoni mwa mambo yanayochochea mgogoro wa Venezuela ni kuongezeka kwa mfumuko wa bei ambao unaelezwa kupanda kwa kasi.

Mbali na mfumuko wa bei, kushuka kwa pato la taifa kulikoanzia wakati wa utawala wa Chavez, na kuendelea hadi sasa, umeliporomosha taifa hilo kiuchumi.

Miaka ya 2000 Chavez akitumia kigezo cha utajiri wa mafuta yaliyopo nchini humo, alikopa kiasi kikubwa cha fedha na sasa deni lake limekuwa mzigo kwa taifa.

Hata hivyo, Maduro amekuwa akiilaumu Marekani na mataifa mengine ya magharibi kuchochea kuidhoofika kwa nchi yake.

Uhaba wa chakula nao umeongezeka ambapo Wavenezuela wanalazimika kula chini ya milo mitatu kwa siku kama inavyoshauriwa kitaalamu.

Utafiti kuhusu hali ya maisha nchi humo uliofanywa mwaka 2017 ulionyesha watu wanane kati ya 10 hawapati mlo kamili huku sita kati ya 10 wakisema wanalazimika kuponea mkate kwa kuwa hawana fedha za kununua chakula kingine.

Changamoto nyingine ni ya uhaba wa huduma za matibabu ambapo inaelezwa katika miaka ya karibuni kumekuwapo na ongezeko la wagonjwa wa malaria na nchi hiyo kuingia katika orodha ya nchi zenye kiwango kikubwa cha ugonjwa huo.

Licha ya kuwa na utajiri wa mafuta, lakini hayaonekani kuwanufaisha Wavenezuela kiuchumi hali inayoamsha hasira za wananchi na kuchochea maandamano ya mara kwa mara kukosoa serikali.

Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na upatikanaji wa huduma, raia wengi wamekuwa wakikimbilia ughaibuni ambapo Hispania, Marekani, Colombia, Brazil, Chile, Peru na Panama ni baadhi ya nchi wanazokimbilia kwa wingi kutafuta maisha bora.