Maseneta wacharuka

Seneta wa Republican, Lindsey Graham akitoa maoni yake kwa waandishi wa habari juzi baada ya kikao cha kupata taarifa juu ya mauaji ya Jamal Kashoggi kutoka kwa Mkurugenzi wa CIA, Gina Haspel. Picha na New York Times   

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  12:43

Kwa Muhtasari

Washangaa namna Rais Trump anavyojaribu kukwepa ukweli

 

Washington, Marekani. Baada ya kikao cha ndani cha kupewa taarifa na Mkurugenzi wa CIA, Gina Haspel Jumanne, maseneta mashuhuri walisema “nafasi ni sifuri” kwamba mrithi wa Ufalme wa Saudia Mohammed bin Salman (MBS) hakuhusika katika mauaji ya mkosoaji Jamal Khashoggi.

“Maoni ambayo nilikuwa nayo kabla yameimarika zaidi,” alisema Seneta Bob Menendez mjumbe wa Kamati ya Seneti ya Uhusiano wa Kimataifa kutoka chama cha Democratic, ambaye ameomba hatua kali kutoka Marekani kuhusu kifo cha Khashoggi na anaunga mkono sheria ya kusitisha msaada kwa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita nchini Yemen.

Seneta wa Republican Lindsey Graham aliwaambia waandishi wa habari, “Unapaswa kwa makusudi kujifanya kipofu ili usifikie hitimisho kwamba tukio hili lilitekelezwa na watu chini ya amri ya MBS.”

Aliongeza kuwa inaonekana utawala wa Trump hautaki kutambua ushahidi wa ushiriki wa mwanamfalme.

Seneta wa Republican Bob Corker, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Uhusiano wa Kimataifa, alitoa maoni kama hayo akisema alikuwa na shaka akilini kwamba bin Salman aliamuru na alikuwa akifuatilia mauaji ya Khashoggi.

Alisema ikiwa mwanamfalme angeshtakiwa kortini, mahakama ingemkuta na hatia katika muda wa “dakika 30 tu”.

Waliopewa taarifa na CIA

Maoni hayo yametolewa baada ya Haspel kuwapa taarifa maseneta wenye ushawishi wa Republican na Democratic ambao ni wajumbe katika Kamati ya Seneti za Huduma ya Silaha, Uhusiano wa Kimataifa, Umiliki na Intelejensia. Maseneta wengine pia walikuwepo.

Maseneta kutoka vyama vyote viwili, wiki iliyopita, walichukizwa na kitendo cha mkurugenzi wa CIA kutohudhuria kikao cha kupewa taarifa kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo na Waziri wa Ulinzi James Mattis. Utawala wa Trump ulikanusha madai kwamba ulimzuia Haspel kuhudhuria.