http://www.swahilihub.com/image/view/-/4925662/medRes/2218095/-/9nfgkmz/-/kabila.jpg

 

Mbivu na mbichi DRC kujulikana baada ya wiki

Rais Joseph Kabila alipokuwa akipiga kura 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  10:19

Kwa Muhtasari

Sehemu kubwa ya kura zilizopigwa hazijahesabiwa mpaka sasa

 

Kinshasa, DRC. Tume ya Uchaguzi (Ceni) ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imesema itatangaza matokeo ya awali baada ya wiki moja kwa sababu mpaka sasa nusu ya kura zilizopigwa bado hazijahesabiwa.

Kituo cha Al Jazeera kiliripoti jana kuwa matokeo ya awali yaliyotakiwa kutangazwa na Ceni Jumapili iliyopita hayakufanikiwa kama ilivyotarajiwa.

Hali imekuwa hivyo kwa sababu sehemu kubwa ya kura zilizopigwa hazijahesabiwa mpaka sasa.

Wananchi wa DRC walipiga kura Desemba 30 kuchagua mrithi wa Rais Joseph Kabila katika uchaguzi ambao wagombea watatu ndio wanaopewa nafasi kubwa ya mmoja wao kuibuka mshindi na hivyo kumrithi Rais Kabila.

Wagombea hao ni mteule wa Rais Kabila, Emmanuel Shadary, Felix Tshisekedi na Martin Fayulu.

Hata hivyo wapinzani wamelalamikia kasoro mbalimbali zilizojitokeza kwenye uchaguzi huo huku wakieleza kwamba Serikali kwa kushirikiana na Ceni wamepanga njama za kuuhujumu uchaguzi huo.

Wiki iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa wito kwa Tume ya Uchaguzi ya DRC kuhakikisha kuwa kura zinahesabiwa kwa umakini na kutishia kuwawekea vikwazo wote watakaohujumu mchakato huo na kutishia amani.

Kwa upande mwingine Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU) waliendelea kutoa msisitizo wa kuitaka nchi hiyo kuheshimu matakwa ya wapigakura wakati muda wa kutangaza matokeo ya uchaguzi ukikaribia.

Kanisa Katoliki nchini humo liliitahadharisha Ceni kuhusu uhesabuji wa kura huku likidai kwamba linamtambua mshindi wa uchaguzi huo na kuwataka watangaze matokeo halisi kama wananchi walivyopiga kura zao.

Hata hivyo, Serikali iliwajia juu viongozi wa kanisa hilo kwa kutumia ushawishi wa kanisa kuchochea wananchi.

Ceni iliahirisha kutoa matokeo ya awali juzi kama ilivyopangwa awali na sasa inasubiriwa kuona matokeo yatakuwaje katika kipinid cha wiki moja yatakapotangazwa.