http://www.swahilihub.com/image/view/-/4930142/medRes/2220866/-/ojpfxh/-/mo.jpg

 

Mo Ibrahim aitaka ICC kumfutia mashtaka Rais Bashir wa Sudan

Mohammed Ibrahim 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  08:46

Kwa Muhtasari

Lengo ni kuzuia umwagikaji wa damu nchini humo.

 

Khartoum, Sudan. Bilionea mashuhuri mzawa wa Sudan, Mohammed Ibrahim ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya Jinai ICC kumfutia mashtaka Rais Omar al-Bashir iwapo atakubali kujiuzulu, kama anavyoshinikizwa na wananchi wanaofanya maandamano dhidi yake tangu mwezi uliopita.

Bilionea huyo ambaye ni mlezi wa Tuzo ya Kifahari ya Mo Ibrahim ambayo hutunukiwa Viongozi wa Afrika walioonesha ukomavu wa kidemokrasia katika utawala wao alisema ili kuzuia umwagikaji wa damu nchini humo ni bora kiongozi huyo akafutiwa mashtaka. “Binafsi napenda kuona watu wakiadhibiwa kutokana na madhambi waliyoyafanya .Ili kukomesha umwagikaji wa damu Sudan kikubwa ni kufutiwa mashitaka na ICC, ni bora jambo hilo lifanyike.”alisema

Waandamanaji wengi wameuawa na wengine kutiwa kushikiliwa tangu wananchi wa maeneo mbalimbali ya Sudan walipoanza maandamano ya kupinga sera za kiuchumi za Serikali ya nchi hiyo Desemba 19 mwaka jana.

Hivi sasa waandamanaji hao wanamtaka Rais al Bashir wa nchi hiyo ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1993 ajiuzulu.

Rais huyo anatuhumiwa na ICC kuwa alihusika na jinai na mauaji ya kimbari Darfur magharibi mwa nchi hiyo mwaka 2003.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi imetoa waranti wa kukamatwa al-Bashir mara mbili, mwaka 2009 na 2010. Hata hivyo nchi nyingi hususan za Afrika zilikataa kumkamata alipozitembelea nchi hizo.

Wafuasi wa Rais waandamana

Ni wiki ya tatu sasa wananchi wakiongozwa na wasomi nchini Sudan kuandamana kumpinga Rais al Bashir hatimaye watu wanaodaiwa kumuunga mkono kiongozi huyo nao waliandamana.

Wafuasi wa Rais Bashir waliandamana mjini Khartoum wakisema wanauunga mkono utawala wake, ambao ulikabiliwa na maandamano makubwa katika wiki za hivi karibuni.

Wakati huohuo vikosi vya usalama vimetumia mabomu ya machozi kwa kutawanya mkusanyiko wa waandamanaji wanaopinga utawala rais huyo.

“Mkusanyiko huu unatuma ujumbe kwa wale wanaofikiri kuwa Sudan itaishia kama nchi nyingine zinazokumbwa na machafuko,” Rais al-Bashir, alisema huku akipongezwa na wafuasi wake.