Mugabe amshusha cheo makamu wake

Robert Mugabe

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe. Picha/HISANI 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  07:38

Kwa Mukhtasari

Rais Robert Mugabe amefanya mabadliko katika Baraza lake la Mawaziri ambako amewaondoa baadhi na kuingiza sura mpya lakini habari kubwa ni kushusha kwa makamu wake Emerson Mnangagwa.

 

HARARE, Zimbabwe

RAIS Robert Mugabe amefanya mabadliko katika Baraza lake la Mawaziri ambako amewaondoa baadhi na kuingiza sura mpya lakini habari kubwa ni kushusha kwa makamu wake Emerson Mnangagwa.

Katika mabadiliko hayo Mnangagwa ambaye alikuwa Waziri wa Sheria sasa atakuwa Waziri wa Utalii hali ambayo imetafsiriwa kama ameshushwa cheo.

Waziri wa Sheria sasa atakuwa Happyton Bonyongwe.

Shirika la Habari la Zimnews likinukuu chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Serikali limesema Mnangagwe alikwishadokezwa kujiandaa kwa makubwa yanayotarajiwa kumfika na sasa amepokonywa nafasi hiyo.

Wakati fulani Mnangagwe alikuwa amepewa nafasi ya kumrithi Mugabe ikiwa tafariki dunia au kuamua kung’a tuka lakini katika siku za karibuni alianza kutopikika na wenzake hasa mke wa Rais Mugabe, Grace Mugabe.

Kilichomponza zaidi ni king’ang’anizi chake kwamba alikula sumu iliyokuwamo kwenye aiskrimu kutoka Kampuni ya Maziwa inayomilikiwa na Grace na akapelekwa Afrika Kusini kwa matibabu.

Rais Mugabe alisema aliambiwa na madaktari waliokuwa wanamtibu Makamu huyo wa Rais kwamba kuugua kwake hakukutokana na sumu lakini yeye anashikilia kwamba alilishwa sumu hali iiyoonyesha kumdhalilisha Rais Mugabe.

Haya yakiwa hivyo, ndani ya Zanu-PF kuna makundi makubwa mawili yanayonyukana kuwania uteuzi wa kugombea urais: La kwanza linaitwa G40 ambako kuna Makamu wa Rais Phelekerzela Mphoko huku kikiungwa mkono na Grace na la pili ni linaitwa Lacoste ambalo linaungwa mkono na Mnangagwe.

Kwa mabadiliko hayo ni kama Makamu huyo wa Rais amepunguzwa kasi.  

Aliyekuwa Waziri wa Fedha Patrik Chinamasa nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani  Ignatus Chombo ambaye ni Katibu Mkuu wa Zanu-PF anayehusika na masuala ya utawala. Wadadisi wa masuala ya siasa wameshtushwa na uteuzi huo wakihoji atafanya nini kuhusu masuala ya  sarafu ya Zimbabwe ambayo inazidi kushuka.

Chinamasa amepewa wizara mpya ya Usalama wa Mitandao.

Muda mfupi baada ya kupewa nafasi, mwigizaji maarufu Carl Joshua Ncube alitania, "Jamani Patrick Chinamasa anawafuatilia kwenye Twitter."

Aliyekuwa Waziri wa Utalii, Walter Mzembi sasa ameteuliwa Waziri wa Mambo ya Nje.