Mugabe na mkewe wakosolewa

Na MASHRIKA

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  14:53

Kwa Mukhtasari

Chama cha Maveterani wa Vita vya ukombozi wa Zimbabwe (ZLWVA) kimesema mashambulizi yanayoelekezwa kwa Makamu wa Rais anayepigwa vita Emerson Mnangagwe na Waziri wa Maveterani aliyeondolewa Tsinga Dube hayawalengi wao tu bali maveterani wote.

 

HARARE, Zimbabwe

CHAMA cha Maveterani wa Vita vya ukombozi wa Zimbabwe (ZLWVA) kimesema mashambulizi yanayoelekezwa kwa Makamu wa Rais anayepigwa vita Emerson Mnangagwe na Waziri wa Maveterani aliyeondolewa Tsinga Dube hayawalengi wao tu bali maveterani wote.

Akizungunza kwenye mkutano wa waandishi wa habari jijini Harare Katibu Mkuu wa ZLWVA, Victor Matemadanda amesema Rais Robert Mugabe na mke wake Gace hawawezi kudai kuwa wana uwezo wa kuwadhibiti wapigania uhuru na chama cha Zanu PF akisema maveterani hao walikwenda vitani kwa hiari yao na sio kujiunga na watu.

Alisema kauli zinazotolewa na Rais Mugabe kwamba maveterani ambao bado wako jeshini hawakuwahi kuwa na jukumu lolote katika chama tawala cha ZANU PF zimeelekezwa kusiko.

“Mashambulizi dhidi ya Makamu wa Rais Mnangagwe na Bwana Tshiba Dube sio tu kwamba yameelekezwa kwao peke yao bali maveterani wote kwa ujumla wao. Tunajua kwamba watajaribu hata kuvuruga mfumo wa jeshi lakini hawawezi kuvuruga historia tuliyoijenga,” alisema Matemadanda.

Matemadanda amesisitiza kwamba  ni maveteran hao walishawishi umma wa watu kukubali kuunga mkono mapambano ya silaha na kwamba  hawakupigania uhuru kwa ajili ya inayoitwa “familia ya kwanza" kufurahia wakati Wazimbabwe wengi wakigalagala kwenye umaskini wa kutupwa.

Alisema hakuna hata mtu mmoja akiwamo Rais Mugabe anayemiliki Zanu PF kwa kuwa chama hicho ni mali ya majeshi ya wapigania uhuru wa ZIPRA na ZANLA pamoja na wananchi wa Zimbabwe.

“Hakuna mtu mwenye mamlaka ya kusema anamiliki ZANU-PF. Wanaweza kusema wanamiliki ZANU Mwenje au ZANU nyingine lakini ZANU PF ni ya kila mmoja. Ikiwa kuna watu wanaodhani wanaweza kutupokonya ZANU-PF hao wanafanya masihara."