http://www.swahilihub.com/image/view/-/1740426/medRes/352794/-/qhevqmz/-/EAMuseveni.jpg

 

Museveni: Kunifanyia masihara ni kosa kubwa

Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Tuesday, November 14  2017 at  15:01

Kwa Mukhtasari

Rais Yoweri Museveni amesema kuwa watu wanaomchukulia kimzaha wanatenda ‘kosa kubwa’ akitolea mfano wa namna alivyotendewa na Chama Tawala cha Uganda People’s Congress (UPC) miaka ya 1980.

 

HOIMA, Uganda

RAIS Yoweri Museveni amesema kuwa watu wanaomchukulia kimzaha wanatenda ‘kosa kubwa’ akitolea mfano wa namna alivyotendewa na Chama Tawala cha Uganda People’s Congress (UPC) miaka ya 1980.

Rais Museveni alitoa mfano wa mambo yaliyo nyuma ya pazia alivyopambana na watu wa nje kuhusu  nini cha kufanya kibiashara na  hazina kubwa ya mafuta itakapogundulika wazi.

Alisema muda mfupi baada ya kushika madaraka mwaka 1986, baadhi ya watu kutoka Ulaya walimfuata ili awaidhinishie kufanya kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta.

Museveni alisema hata hivyo aliwakataila na badala yake aliamua  kuwapeleka Waganda kusomea uchumi wa mafuta na gesi ili kujenga uwezo kabla ya kuanza kazi ya uchimbaji.

“Mimi sitaniwi,” alisema Rais Museveni “Hata UPC walifanya kosa hilo.”

Mwaka 1980 Museveni ambaye aligombea urais kwa tiketi ya ‘Uganda Patriotic Movement (UPC)’ alionya kuwa atakwenda msituni ikiwa uchaguzi utavurugwa.

Milton Obote alishinda hivyo akarudi kuiongoza Uganda kwa mara ya pili baada ya kupinduliwa na Idd Amin Mwaka 1971.

Museveni alianzisha vita vya msituni dhidi ya Serikali ya Obote iliyopinduliwa na Tito Okello Lutwa ambaye pia yake ilipinduliwa na Museveni mwaka 1986.

Rais akizungumza Jumamosi iliyopita wakati wa sherehe fupi za usinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta Afrika Mashariki alitaja umuhimu wa kubuni vyanzo vya uchumi akisema wanaofanya masihara naye wanatenda kosa kubwa.

Mradi wa ujenzi wa boma utakapokamilika utakuwa unasafirisha mapipa ya mafuta kutoka Hoima kwenda Bandari ya Tanga kabla ya kusafishwa nje ya nchi.