Mwandishi CNN amtoa povu Trump

Mwandishi wa habari wa CNN, Jim Acosta akikataa kumpa kipaza sauti Ofisa wa Ikulu ya Marekani baada ya kuamriwa na Rais Trump (kulia) kufanya hivyo  

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  12:25

Kwa Muhtasari

Ni baada ya kuuliza maswali aliyoshindwa kujibu

 

Washington, Marekani. Maofisa wa Ikulu ya Marekani wamemzuia mwandishi wa Kituo cha televisheni cha CNN anayehusika na habari za Ikulu, Jim Acosta kuandika habari za Rais wa Marekani, Donald Trump.

Mwandishi huyo amezuiwa kuandika tena habari zinazomhusu Rais Trump kwa kile walichokisema kwamba amemuuliza Rais swali lisilofaa.

Acosta alitaka kufahamu hatma ya wahamiaji zaidi ya 4,000 wa Amerika ya Kati ambao wanatembea kupitia Mexico kuomba hifadhi Marekani. Ghafla Rais Trump akamjibu kifupi kwamba “Tunaenda’’

Acosta alipinga matumizi ya maneno ambayo Trump huwa anayatumia kwa wahamiaji hususan neno uvamizi, Trump akamwambia “Unataka waje kwa kuvunja sheria.’’

Wakati Trump alipotaka kumruhusu mwandishi mwingine Acosta alikataa kurudisha kipaza sauti na kuendelea kuuliza maswali mengine.

Akitaka kujua alipofikia mchunguzi maalumu Robert Mueler kuhusu uchunguzi wa kilichotokea wakati wa kampeni 2016.

Trump hakuweza kujibu swali hilo huku akimtaka kuweka chini kipaza sauti “Weka chini hicho kipaza sauti’’ aliamrisha hapo ndipo wasimamizi wa mkutano wakiwamo maofisa wa Ikulu walipolazimika kumtoa nje lakini akawa anagoma.

Acosta alituma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter Jumatano jioni akisema kwamba Ofisa wa Ikulu aliyemtoa kwenye mkutano hana makosa kwani alikuwa akifanya kazi yake.

“Najua alikuwa akifanya kazi yake, hivyo siyo kosa lake,’’aliandika Acosta

“Ukweli kuwa CNN inajivunia kile mfanyakazi wao alifanya sio tu cha kughadhabisha, ni mfano wa kukosa heshima kwa kila mtu, akiwemo mwanamke ambaye anafanya kazi katika uongozi huu,” alisema Trump

Msimamizi wa mkutano huo Sarah Sanders aliandika kwenye mtandao kwamba mwandishi huyo anatakiwa kuacha mara moja kuandika habari za Ikulu kwa sababu alikataa kurudisha kipaza sauti kama alivyotakiwa.

Alisema mwandishi huyo alikataa kurudisha kipaza sauti kama alivyoamriwa na Rais Trump huku akimzuia kwa mkono ofisa wa Ikulu aliyekuwa anatakiwa kuchukua kipaza sauti hicho kama alivyoamriwa.

Januari mwaka huu

Rais alichukizwa na maswali ya mara kwa mara kuhusu kauli yake ya kuita Mataifa ya Afrika kuwa machafu.

Pia alimuuliza kwamba anapendelea wahamiaji kutoka nchi za watu weupe au jamii ya kihindi. Trump akajibu nje,

Trump na Acosta pia waliwahi kukwaruzana baada ya kuchapishwa kwa nyaraka kuhusu uhusiano na Russia huku Trump akisema “Nyinyi mnaandika habari za kubuni’’