Mwenendo wa uchaguzi DRC wamchefua Papa

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis 

Imepakiwa - Wednesday, January 9  2019 at  09:08

Kwa Muhtasari

Awataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanaheshimu sheria za uchaguzi

 

Kinshasa, DRC. Baada Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (Ceni) kutangaza kuahirisha kutoa matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis ameitaka Serikali na Tume hiyo kuhakikisha kunakuwa na amani.

Papa aliwataka viongozi wa nchi hiyo na wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha mwisho wa mchakato wa matokeo kuna- kuwa na amani nchini humo.

“Ninatoa tahadhari kufuatia mabadiliko ya hali nchini DRC, nchi hiyo inaweza kabisa kurejesha upatanisho wa muda mrefu,” ilisema Papa kupitia taarifa yake.

Aliwataka wahusika wa usimamizi wa uchaguzi huo kuhakikisha wanaheshimu sheria za uchaguzi bila kuvunja utaratibu kwani ikiwa kutatokea machafuko wanaoathirika zaidi ni wazee na watoto.

UN waahirisha mkutano

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeahirisha mkutano muhimu kuujadili uchaguzi wa nchi hiyo jana kutokana na Afrika Kusini kuwasilisha ombi hilo baada ya Serikali ya DRC kutangaza kuwa matokeo yatachelewa kutolewa.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia, baraza hilo la usalama lilikuwa likutane jana kuijadili nchi hiyo, lakini sasa mkutano huo utafanyika Ijumaa ijayo.

Ijumaa iliyopita baraza hilo lilifanya mkutano wa faragha baada ya Ufaransa kutoa ombi, lakini mataifa yenye nguvu duniani yalishindwa kukubaliana kuhusu tamko la kutoa kabla ya matokeo kutangazwa.

Maaskofu

Baada ya kumalizika upigaji kura, Baraza Kuu la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (Cenco) lilisema mashine za kupigia kura zilikumbwa na hitilafu katika takriban vituo 544 kati ya 12,300 katika maeneo waliyofuatilia upigaji kura. Maaskofu hao waliwataka watawala nchini humo kuwa wakweli na kutangaza matokeo.

Baadhi ya wapiga kura walilalamika kwamba majina yao hayakupatikana kwenye daftari la wapiga kura.

Rais mteule wa nchi hiyo anatarajiwa kutangazwa Januari 15 na kuapishwa Januari 18.