http://www.swahilihub.com/image/view/-/4802388/medRes/2138198/-/hyjb53/-/oby.jpg

 

Nigeria yaandika historia mpya mwanamke kuwania urais

Oby Ezekwesili  

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  09:11

Kwa Muhtasari

Kujitokeza kwake kunadaiwa kuongeza mwamko wa kisiasa nchini humo

 

 

Lagos, Nigeria. Oby Ezekwesili ni mwanamke maarufu nchini Nigeria aliyeamua kujiingiza katika ulimwengu wa kisiasa kwa kuwania urais katika taifa ambalo kwa miaka mingi ni wanaume ndio wanaozihodhi siasa za nchi hiyo.

Ezekwesili aliongoza kampeni ya kimataifa ya kutaka waachiwe huru wasichana wa shule ya Chibok waliotekwa nyara na kundi la itikadi kali la Boko Haram sasa ameamua kugombea urais nchini Nigeria.

Aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia (Afrika) na pia ni mwasisi mwenza wa Shirika la Kimataifa la Transparency ambalo liko mstari wa mbele katika kuipiga vita rushwa duniani.

Inatajwa kwamba tatizo kubwa linaloisumbua nchi ya Nigeria ni rushwa licha ya kuwa na utajiri wa mafuta.

Lakini pengine Oby anafahamika zaidi hasa katika mapambano yake ya kupigania kuachiwa huru wasichana wa shule waliotekwa nyara na kundi la wanamgambo wa Boko Haram linalotumia kisingizio cha dini ya kiislamu kuendeleza uovu na ukatili.

Kundi hilo liliwateka nyara wasichana zaidi ya 200 wa shule kutoka jamii ya Wachibok mwaka 2014.

Kampeni aliyoianzisha Ezekwesili iliungwa mkono hata na aliyekuwa mke wa rais wa zamani wa Marekani, Michelle Obama pamoja na viongozi wengi mashuhuri ambao waliishinikiza bila kuchoka Serikali ya Nigeria kuweka msukumo wa kuachiwa huru kwa watoto hao wa kike.

Rais Mohammadu Buhari aliyetoa ahadi ya kupambana na Boko Haram pamoja na rushwa alipoingia madarakani mwaka 2015 ambako Serikali yake ilijitapa kuwa mshindi katika kisa hicho cha kuachiwa huru wasichana wa Chibok dhidi ya Boko Haram.

Hata hivyo Ezekwesili anataka kupambana na rais huyo mwenye umri wa miaka 75 na anampa changamoto hasa kuhusiana na ahadi alizozitoa katika kampeni zake wakati akiwania kiti cha urais.

Mapambano hayo ni kuelekea uchaguzi wa Rais utakaofanyika Februari mwaka 2019.

Hata hivyo lipo tatizo jingine kubwa Nigeria la mtizamo uliopo kuhusu wagombea wanawake na hasa kwa sababu raia wengi nchini humo wanahisi mwanamke anatakiwa kufanya kazi za jikoni pekee.

Na hata Rais Buhari mwenyewe aliwahi kusema akiwa amesimama pembeni ya mwanamke mwenye nguvu duniani Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kwamba yeye ana maarifa makubwa kuliko mkewe ambaye anafahamu mengi kuhusu jikoni, sebuleni na kwengineko.

Marais ambao waliwahi kuitalawa Nigeria ni pamoja na Sani Abacha, Nnamdi Azikiwe, Ibrahim Babangida, Olusegun Obasanjo, Shehu Shagari na Ernest Shonekan na sasa Muhammadu Buhari.

Kujitokeza kwa mgombea huyo kunadaiwa kumeongeza mwamko wa kisiasa nchini humo.