Obama na familia wafurahia maisha baada ya urais

Na  MASHIRIKA

Imepakiwa - Thursday, February 2  2017 at  20:42

Kwa Muhtasari

RAIS wa Amerika aliyeondoka Barack Obama ameonekana kufurahia maisha yake ya uraia akiwa likizoni na familia yake.

 

Picha zilizochapishwa na shirika la habari la Daily Mail zilimwonyesha rais huyo wa kwanza mweusi wa Amerika akiwa amebadilika na kurejelea hali yake ya zamani kabla alipokuwa rais.

Picha hizo zilimwonyesha akiwa amevaa kandambili miguuni, surwali fupi na kofia iliyopinduliwa kinyumenyume.

Mke wake, Michelle Obama pia alikuwa amevaa mavazi yaliyomfanya aonekane tofauti sana na alivyokuwa wakati walipoishi katika Ikulu ya White House.

Imeripotiwa wawili hao wako likizoni katika kisiwa kinachomilikiwa na mwekezaji bilionea Richard Branson ambaye ni rafiki wa familia yao. Branson humiliki visiwa viwili, cha Necker na Moskito na imedaiwa familia ya Obama iko Moskito ingawa hayo hayajathibitishwa.

Kulingana na mashirika ya habari,  wafanyakazi katika kisiwa ambako wanaishi walipigwa marufuku kuingia na simu zao za rununu hadi familia hiyo itakapokamilisha likizo yao.

Licha ya uraia wake, imesemekana aliandamana na karibu wasaidizi 100 wengi wao wakiwa walinzi wa idara ya Secret Service iliyo na jukumu la kulinda viongozi wa kitaifa.

 

 

Imekusanywa na VALENTINE OBARA