Panya aongezwa Oksijeni kuokoa maisha yake

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Sunday, October 30  2016 at  18:18

Kwa Muhtasari

SOUTHAMPTON, UINGEREZA

MAAFISA wa zimamoto walishangaza kwa kumwokoa panya buku kutoka kwa nyumba iliyokuwa ikichomeka na kumpa matibabu kana kwamba ni binadamu.

 

Picha zilienezwa mitandaoni kuonyesha jinsi panya huyo alivyookolewa na kuongezewa oksijeni ili kumpunguzia madhara ambayo yangetokana na uvutaji wa moshi mkali. Aliwekewa vifaa puani kumwongeza hewa safi.

Afisa kutoka kwa idara ya zimamoto ya Redbridge Bw Steve Crammer alinukuliwa kusema: “Alikuwa anatetemeka na kupata matatizo makubwa ya kupumua kwa hivyo tulimtengezea sehemu ndogo kwenye kisanduku cha vifaa vyetu ili alale kidogo.”

Alipatikana akiwa tayari ameanza kugeuka rangi kwa kukosa hewa safi lakini maafisa walieleza matumaini kuwa atapona.

Kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, shirika la huduma za ambulensi la NHS Foundation Trust lilisema:

“Wote waliokuwemo walipatikana wakiwa salama ingawa haka kajamaa kadogo kalihitaji matibabu ya oksijeni kutokana na moshi aliovuta. Tunatarajia atapona kikamilifu.”

 

Imekusanywa na Valentine Obara