Raia wa Catalonia waandamana wakitaka viongozi waachiliwe huru

Na AFP

Imepakiwa - Sunday, November 12  2017 at  16:54

Kwa Muhtasari

MAMIA ya maelfu ya wakazi wa jimbo la Catalonia waliandamana Jumamosi kutaka viongozi wa eneo hilo ambao walikamatwa kwa kushinikiza jimbo hilo lijitenge waachiliwe huru.

 

Maandamano hayo ya zaidi ya saa mbili jijini Barcelona, ambako ni makao makuu ya Catalonia, yalifanyika siku moja pekee baada ya spika wa bunge la jimbo hilo, ambaye alisimamishwa kazi na serikali kuu mwezi uliopita, kuachiliwa huru.

Alikuwa amekamatwa pamoja na maafisa wengine wengi wa Catalonia, akaachiliwa baada ya kulipa dhamana ya dola 175,000 (Sh18.03 milioni).

Waandamanaji walikusanyika katika barabara iliyopakana na bunge la eneo hilo wakipeperusha bendera za uhuru wa Catalonia na kusema “Uhuru!” huku wengine wakibeba mabango yaliyotoa wito wa demokrasia.

Watoto pia hawakuachwa nyuma kwenye maandamano hayo. Baadhi yao waliovaa helmeti walibebana mabegani kuchora mchoro wa kasri huku wengine wakibeba mabango yenye michoro ya baadhi ya wabunge wao ambao wangali kizuizini.

Polisi wa manispaa ya Barcelona walikadiria kuwa kulikuwa na waandamanaji wasiopungua 750,000 ambao walijaa umbali wa zaidi ya kilomita 15.

Mgogoro wa Catalonia umesababisha wasiwasi katika Muungano wa Ulaya ambao tayari unakumbwa na matatizo kuhusu jinsi Uingereza ilivyojiondoa EU, ikizingatiwa kuna wakazi milioni 7.5. Zaidi ya biashara 2,400 tayari zishahamisha makao yao makuu kutoka jimbo hilo.

Jumatano iliyopita, mgomo ulioitishwa na vyama vya wafanyakazi vinavyounga mkono eneo hilo kujitenga ulisababisha changamoto za usafiri kwani barabara 60 zilizibwa pamoja na reli, ikiwemo barabara kuu inayounganisha Uhispania na Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya.

Catalonia ni eneo lenye utajiri mkubwa ambalo lina lugha yake na tamaduni za kipekee.

Tangu wabunge wa jimbo hilo walipotangaza uhuru Oktoba 27 baada ya kufanya kura ya maoni iliyopigwa marufuku na serikali kuu, maafisa waliounga mkono hatua hiyo wamekuwa wakiandamwa sana na serikali kuu iliyo na makao yake makuu mjini Madrid.

Serikali kuu ilimpuuzilia mbali kiongozi wa Catalonia, Carles Puigdemont, serikali yake na bunge. Ilifutilia mbali uhuru wa eneo hilo na kuagiza uchaguzi mpya ufanyike Desemba 21.

Awali, Meya wa Barcelona, Ada Colau, alikashifu hatua za serikali ya Puigdemont.

“Wamesababisha taharuki na kutangaza uhuru kivyao ilhali watu wengi hawataki kuwe hivyo. Wamehadaa wakazi kwa manufaa yao ya kibinafsi,” akasema.

Puigdemont alitorokea Ubelgiji akisubiri kesi inayotaka arudishwe Uhispania isikilizwe. Serikali kuu ilitoa agizo la kukamatwa kwake kwa mataifa yote ya EU.