Raila ajiondoa urais 2022

Raila Odinga  

Imepakiwa - Wednesday, November 7  2018 at  10:18

Kwa Muhtasari

Badala yake anataka kujikita kwenye kazi mpya katika Umoja wa Afrika

 

Nairobi, Kenya. Kiongozi wa muungano wa upinzani wa Nasa na aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita Raila Odinga amejiondoa katika siasa za kurithi madaraka mwaka 2022 na badala yake anataka kujikita kwenye kazi mpya katika Umoja wa Afrika.

Katika taarifa rasmi iliyosambazwa Jumatatu, msemaji wake Dennis Onyango amesema Odinga atakuwa katika mapumziko yanayoambatana na malipo na kwamba hatajihusisha na siasa zinazozungumzia kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

“Ili aweze kuonyesha uongozi unaohitajika katika eneo hili na kwa kuzingatia matamko ya siku za nyuma, Odinga anapenda kusisitiza kwamba hatajihusisha na siasa za kurithishana kuelekea mwaka 2022,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Imeelezwa kwamba waziri mkuu huyo wa zamani ameamua kujikita katika utekelezaji wa majukumu yake kama mjumbe maalum.

“Odinga anataka kuelekeza nguvu zake kwa miaka ijayo katika ujenzi wa miundombinu barani Afrika kupitia majukumu ya ofisi yake mpya na kuwaunganisha Wakenya kupitia Mpango wa Ujenzi wa Madaraja,” alieleza msemaji wake.

Onyango alifafanua kuwa Raila ataelekeza macho yake katika mpango wa ujenzi wa madaraja, mkakati uliozaliwa tangu aliposhikana mkono na Rais Kenyatta.

Maswali yameibuka ikiwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao cha Odinga, Uhuru, na Ruto ambaye imeripotiwa anajipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa rais mwaka 2022.

Baada ya uamuzi huo chama kikuu cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) kinatarajia kujipanga upya ili kumpata mtu atakayevaa viatu vya Raila.

Seneta wa Siaya James Orengo, ambaye ni mshirika wa karibu wa kiongozi huyo wa upinzani, anatajwa kuwa mshindani wa juu wa kujaza nafasi hiyo.

Alichosema 2017

Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2017, Raila alisema ikiwa angeshindwa kihalali angestaafu siasa. Lakini baada ya uchaguzi ule uliofutwa na kutangazwa wa marudio mwanasiasa huyo alimshutumu Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa matamshi yao kwamba ni “mzee hivyo anapaswa kustaafu siasa”.

Jumapili ya Oktoba 29, waziri mkuu huyo wa zamani alisema atastaafu tu siasa baada ya kuwawezesha Wakenya “kuondokana na serikali ya kifisadi ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta” au pale moyo wake ukiridhia.

“Wanataka nistaafu kwa sababu umri wangu mkubwa lakini nataka Wakenya waelewe kuwa nitaachana na siasa siyo kwa sababu Uhuru na Ruto wanataka nifanye hivyo, bali kwa kuwa nitakuwa nimefanikisha Wakenya kuungana,” alisema Odinga mwenye umri wa miaka 73.