http://www.swahilihub.com/image/view/-/4759456/medRes/2109762/-/uwbq6q/-/uhuru.jpg

 

Rais Kenyatta apunguza VAT kutoka asilimia 16 hadi 8 kwa bidhaa za petroli

Rais Uhuru Kenyatta  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  15:43

Kwa Muhtasari

Utozaji ushuru kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa ulisababisha gharama ya maisha kuongezeka


 

Nairobi, Kenya. Wakenya wamepata afueni kiasi baada ya Rais Uhuru Kenyatta Ijumaa kupendekeza kupunguzwa utozaji ushuru, VAT ya asilimia 16 kwa bidhaa za petroli hadi asilimia 8.

Tangazo hilo limejiri siku moja baada ya kiogozi huyo wa taifa kukataa kutia saini mswada wa Bili ya 2018 uliopitishwa na bunge wiki kadhaa zilizopita, wenye kipengele kilichopendekeza kuahirishwa kwa VAT hiyo kwa muda wa miaka miwili ijayo.

Hazina ya Kitaifa iliagiza tume ya kudhibiti kawi nchini (ERC) kutekeleza utozaji wa ushuru huo kuanzia Septemba 1, lakini bunge likapitisha mswada wa kuuahirisha hadi 2018. Rais Kenyatta hata hivyo, Alhamisi alirejesha mswada huo bungeni akipendekeza ufanyiwe marekebisho.

Kenyatta akihutubia taifa katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi, alisema ushuru unaotozwa Wakenya ndio hutumika kufanya maendeleo. "Maendeleo yote tunayofanya hutegemea ushuru tunaowatoza. Kufuatia VAT ya asilimia 16 kwa bidhaa za petroli, ninatangaza kuipunguza hadi asilimia 8. Hii ina maana kuwa endapo bunge litakubali, lita moja ya mafuta ya petroli itashuka kutoka Sh127-118, na dizeli kutoka Sh115-107," akafafanua.

Hata hivyo, Rais alionya wafanyabiashara kukoma kukandamiza wananchi kwa kutumia kigezo cha mafuta kutozwa ushuru na kuongeza bei ya bidhaa kiholela.

Utozaji ushuru kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa ulisababisha gharama ya maisha kuongezeka, ambapo baadhi ya bidhaa ziliongezwa bei pamoja na nauli. VAT kwa bidhaa hizo imekuwa ikitozwa licha ya mahakama kuu kuagiza isitishwe.

Ushuru huo unatokana na shinikizo la shirika la kimataifa la kifedha (IMF) kwa serikali ya Kenya, lililoishauri kutoza bidhaa za petroli, kupunguza gharama ya matumizi kwa watumishi wa umma, ili kumudu kulipa mikopo inayotumika kufanya maendeleo.

Mikopo hiyo inaendelea kuongezeka, maswali chungu nzima ya matumizi yake yakiibuliwa. Mjadala wa VAT kwa bidhaa za petroli ulianza 2013, ambapo pendekezo hilo liliahirishwa kwa muda wa miaka mitatu, hadi 2016. Muda huo ulipokamilika, wabunge walipitisha mswada wa kuliahirisha hadi Septemba 1, 2018. Rais Kenyatta kwenye hotuba yake, alionekana kucharura Bili ya 2018, akiitaja kama "Inayolenga kuzima ndoto za maendeleo kwa Wakenya".

Aliorodhesha miradi kama; reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi maarufu kama SGR, masomo bila malipo katika shule za msingi na upili, huduma za uzazi bila malipo katika hospitali za umma, bima ya afya (NHIF), ujenzi wa barabara na uwekaji wa stima, kama maendeleo yaliyofanikishwa na ushuru unaotozwa wananchi.

Alisema katiba iliyozinduliwa mwaka 2010 imesaidia kuendesha mbele taifa, ambapo linajivunia kwa ugatuzi. "Zaidi ya Sh1 trilioni tumezituma kwa serikali za kaunti tangu 2013 ili kufanya maendeleo," akasema.

Kenyatta pia alisema gharama ya matumizi katika taasisi za serikali itapunguzwa, ili kupunguza gharama kwa walipa ushuru. Alisisitiza kuwa serikali yake itaendelea na vita dhidi ya ufisadi kwa madhumuni ya kunusuru mali ya umma inayofyonzwa na watumishi wenye tamaa za ubinafsi. "Serikali itaongeza mgao wake wa ufadhili kwa idara ya mahakama na ofisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma (ODPP), ili wapambane na ufisadi vilivyo," akafafanua.

Tangu ahifadhi kiti chake 2017, Rais Kenyatta amekuwa mstari wa mbele kupambana na visa vya ufisadi nchini ambapo taifa limeshuhudia baadhi ya viongozi wakuu serikalini wakifikishwa mahakamani, na kufunguliwa mashtaka kwa kuhusishwa na sakata za ubadhirifu wa mali ya umma.