http://www.swahilihub.com/image/view/-/4340694/medRes/1454127/-/8mjyerz/-/antonio.jpg

 

Antonio Guterres afurahia kujitolea kwa Rais Kenyatta na Raila kushirikiana kuifaa Kenya

Antonio Guterres

Katibu Mkuu UN, Antonio Guterres akiwa katika afisi za UN jijini Geneva awali. Picha/MAKTABA 

Na WAANDISHI WETU

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  11:42

Kwa Muhtasari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, asema amefurahia kujitolea kwa Uhuru na Raila kufanya kazi pamoja; ahidi kwamba UN ipo kwa ajili ya kusaidia kuhakikisha amani inadumu, kuna uthabiti na maendeleo Kenya.

 

UMOJA wa Mataifa (UN) Jumanne ulisifu mkutano wa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga, ukisema hio ilikuwa hatua muhimu ya kuwaunganisha Wakenya.

Guterres alisema umoja huo ulifurahishwa na juhudi hizo ulizozitaja kama hatua muhimu ya kutuliza joto la kisiasa nchini.

“Nasisitiza ahadi ya UN kuendelea kushirikiana na serikali ya Kenya pamoja na raia wa Kenya katika juhudi zakuleta umoja, amani na maendeleo,” Bw Guterres alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Siku chache kabla ya Bw Odinga kujiapisha kama 'Rais wa Wananchi’, UN ilimtuma aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo kuanzisha mdahalo wa kisiasa nchini lakini juhudi hizo zikagonga mwamba.

Katika kikao na wanahabari mjini Geneva mnamo Januari 19, 2018, msemaji wa Guterres Bw Stephane Dujarric alisema: “Kama mnavyofahamu hali ya kisiasa nchini Kenya ni suala tunalofuatilia kwa makini sana, haswa mpango wa kinara wa upinzani kujiapisha mwisho wa Januari. Ni katika muktadha huo ambapo Bw Obasanjo alitumwa kuzuru Kenya.”

Juhudi za Bw Obasanjo hata hivyo zilipingwa vikali na viongozi wa Jubilee na wale wa Nasa.

Baada ya msururu wa visa vya baadhi ya viongozi wa upinzani kukamatwa na stakabadhi zao za usafiri kutwaliwa na serikali, Ijumaa iliyopita Rais Kenyatta na Bw Odinga walishiriki kikao cha ghafla na kutangaza kufanya kazi pamoja.

Wawili hao walitangaza ajenda yao ya kuunganisha Wakenya pamoja na kuanzisha mchakato wa kutatua masuala nyeti ya kitaifa.

Bw Guterres alisema UN inaunga kikamilifu juhudi za wawili hao na kuwataka raia wa Kenya kuwapa nafasi ya kutekeleza waliokubaliana.

Haya yanajiri huku vinara wenza wa NASA Kalonzo Musyoka, Musalia Muadvadi na Moses Wetangula wasisitiza kufanyika kwa mdahalo unaohusisha viongozi wote.

Jumanne, baadhi ya viongozi wa Ukambani waliunga mkono hatua ya Rais Kenyatta na Bw Odinga na kuwakashifu vikali wanaopinga umoja huo.

Wakiongozwa na aliyekuwa Seneta wa Kitui David Musila, viongozi hao waliwataka wanasiasa wa pande zote kuunga mkono juhudi hizo bila kuweka masharti.