http://www.swahilihub.com/image/view/-/4605900/medRes/2004446/-/10tk5ydz/-/chuwema.jpg

 

Rais Trump azifungulia taasisi za Serikali

Donald Trump

Rais Donald Trump wa Marekani ajibu maswali yaliyoulizwa na wanahabari wakati wa mkutano wa mataifa yenye nguvu kiviwanda G7 Juni 9, 2018, mjini La Malbaie, Quebec, Canada. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Monday, January 28  2019 at  14:59

Kwa Muhtasari

Suala la ukuta baina ya mpaka wa Marekani na Mexico lingali halijapatiwa suluhu.

 

WASHINGTON DC, Marekani

RAIS wa Marekani, Donald Trump ametangaza kufunguliwa kwa idara za serikali kuu ambazo zilifungwa kwa zaidi ya mwezi mmoja, baada ya kufikia makubaliano na kamati ya pamoja ya Bunge.

Makubaliano yaliyofikiwa wiki iliyopita yataruhusu idara za Serikali Kuu kufunguliwa kwa kipindi cha wiki tatu mpaka Februari 15, wakati ambapo majadiliano yataendelea kufanyika kuhusu suala kuu la ulinzi wa mpaka.

Vyanzo vya habari katika Bunge la Marekani - Congress vinasema kuwa makubaliano yaliyofikiwa hayajumuishi fedha za ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.

Rais Donald Trump amesaini makubaliano ya kufungua tena Serikali ya Marekani kwa kipindi cha wiki tatu; baada ya kuvunja rekodi ya kufungwa idara hizo za Serikali Kuu kwa muda mrefu kuliko wakati wowote.

Rais Trump amesema kuwa mkataba huo uliofikiwa utaiwezesha Serikali kuendesha shughuli zake hadi Februari 15.

Alisema kuwa wafanyakazi wa Serikali Kuu watalipwa mshahara wao wote “kwa haraka iwezekanavyo.”