http://www.swahilihub.com/image/view/-/4924220/medRes/2217193/-/19ty4fz/-/viongozi.jpg

 

Serikali DRC yalijia juu kanisa

Viongozi wa Kanisa Katoliki wa Jamhuri ya Congo (DRC) wakitoa taarifa kwa waandishi juzi. 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  10:06

Kwa Muhtasari

Baraza la maaskofu limeonya likisema watuhumiwa wa kwanza ni Tume ya Uchaguzi (Ceni)

 

Kinshasa, DRC. Vuguvugu kubwa limeibuka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kati ya Serikali na uongozi wa Kanisa Katoliki baada ya Tume ya Uchaguzi kusitisha kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi huku kanisa hilo likisema linamfahamu mshindi.

Pia kumekuwa ongezeko la shinikizo kutoka mataifa yenye nguvu na Kanisa Katoliki kuitaka nchi hiyo kuheshimu matakwa ya wapiga kura.

Serikali imekemea ushawishi unaotolewa na kanisa hilo unaodai kuwa wanajua kiongozi aliyeshinda katika uchaguzi wa rais.

Baraza la Maaskofu, (Cenco), limeonya kwamba hasira za umma zinaweza kujitokeza iwapo matokeo ya mwisho hayatakuwa ya kweli kwa mujibu wa matokeo halisi ya kura.

Barua iliyoandikwa kwa Tume ya Uchaguzi nchini humo kutoka kwa rais wa baraza la Cenco, Marcel Utembi ilisema kwamba kutokana na ucheleweshaji wa matokeo, “Iwapo kutakuwa na vuguvugu la maandamano ya umma itakuwa ni jukumu la Ceni.”

Barnabe Kikaya Bin Karubi ambaye ni msemaji wa ‘Common front for the Congo’, ameiambia BBC kuwa “Jambo linalofanywa na kanisa ni kitu ambacho hakikubaliki, ni sawa na kuwaandaa watu kufanya mapinduzi”.

Serikali ya mseto imesisitiza kwamba ni Tume ya Uchaguzi peke yake ndiyo inayoweza kutangaza matokeo ya uchaguzi.

Kanisa linamjua mshindi

Kanisa hilo lenye ushawishi nchini humo ambalo limetoa zaidi ya wachunguzi wa uchaguzi 40,000, lilisema kwamba linamjua mshindi wa uchaguzi huo lakini halikumtaja.

Uchaguzi huo wa Desemba 30 ulishuhudia wagombea 21 wakipambana kuwania kuchukua nafasi ya Rais Joseph Kabila ambaye ameitawala nchi hiyo iliyokumbwa na mizozo kwa karibu miaka 18.

Miongoni mwa wale waliopo katika nafasi za mbele ni pamoja na mrithi aliyeteuliwa na Kabila Emmanuel Ramazani Shadary na wagombea wawili wa upinzani, mwanasiasa wa siku nyingi mwenye ushawishi mkubwa Felix Tshisekedi na Martin Fayulu ambaye amejitokeza hivi karibuni.

Anayetafutwa ni mwanasiasa kiongozi katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini ambayo haijawahi kuwa na kipindi cha madadiliko ya amani ya utawala tangu kujipatia uhuru kutoka Ubelgiji mwaka 1960.

Kabila alipaswa kuondoka madarakani miaka miwili iliyopita, lakini aling’ang’ania madarakani na kusababisha maandamano ambayo yalisababisha watu wengi kupoteza maisha.

Uchaguzi, ambao ulitanguliwa na kucheleweshwa mara kwa mara, ulifanyika katika hali ya utulivu. Lakini hali ya wasi wasi imejijenga katika muda wa kipindi cha mchakato wa kuhesabu kura, huku kukiwa na hofu kwamba matokeo yanaweza kuchakachuliwa ili kumuweka Shadary madarakani.

Matokeo ya awali, ambayo yalipangwa kutolewa jana sasa yatatolewa wiki hii, Mkuu wa Tume ya Uchaguzi nchini humo, Corneille Nangaa aliliambia Shirika la Habari la AFP.

Nangaa pia alisema kwamba matokeo zaidi ya asilimia 80 ya kura bado yanasubiriwa.

Rais Kabila anatarajiwa kuondoka madarakani baada ya kuongoza nchi hiyo kwa takriban miaka 17 na ameahidi kukabidhi madaraka kwa atakayeshinda uchaguzi.

Kabila awali alitarajiwa kuondoka madarakani mwaka 2016 lakini uchaguzi ukaahirishwa kutokana na kile ambacho Serikali yake ilisema ni kutokamilika kwa maandalizi.

UN wakutana

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekutana juzi katika kikao cha faragha ili kujadili uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo na hali ilivyo mpaka sasa.

Mkutano huu uliombwa kufanyika na nchi ya Ufaransa wakati huu Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Umoja wa Afrika (AU) wakizitaka mamlaka nchini humo kuheshimu matokeo ya uchaguzi huo.

Marekani imetoa wito matokeo sahihi ya uchaguzi yatangazwe na kuwataka viongozi wa nchi hiyo waondowe vizuizi vilivyowekwa dhidi ya mitandao.

Nchi za Magharibi kwa pamoja na nchi jirani na DRC zimeelezea matumaini yao kuiona nchi hiyo kubwa kabisa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara ikishuhudia kipindi cha mpito katika mazingira ua amani na usalama.

Wagombea wakuu

Kulikuwa na wagombea 22 lakini waliokuwa na nguvu na wanaotajwa kwamba kuna mmoja huenda akaibuka mshindi ikiwa uchaguzi utaenda vizuri ni watatu tu

Wagombea hao ni Emmanuel Shadary, Waziri wa zamani wa mambo ya ndani na mtiifu kwa Kabila, ambaye aliwekewa vikwazo na Muungano wa Ulaya kwa hatua zilizochuliwa dhidi ya upinzani wakati wa maandamano ya mwaka 2017. Shadary anatajwa kuwa ndiye chaguo la Kabila

Mgombea mwingine ni Martin Fayulu, huyu ni mkurugenzi mkuu wa zamani wa mafuta ambaye ameahidi kuifanya DRC iwe nchi yenye mafanikio lakini ambaye watu maskini wanahisi hawezi kuwatetea.

Katika mbio hizo pia yumo, Felix Tshisekedi, huyu ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe marehemu, Etienne Tshisekedi. Katika kampenzi zake Felix ameahidi kupambana na umaskini.