Shambulizi la kombora laua watu 3 Mogadishu

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Thursday, February 16  2017 at  21:39

Kwa Mukhtasari

Takriban watu watatu wakiwemo watoto wawili waliuawa na wengine watano wakajeruhiwa waliposhambuliwa kwa kurushiwa kombora katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

 

Kisa hicho kilitokea Alhamisi Februari 16, 2016. Shambulizi hilo lilitokea katika Wilaya ya Warta Nabada ambako Ikulu ya rais imo kwa mujibu wa polisi.

Sajini wa polisi Ali Ahmed alithibitisha kisa hicho kwa kusema makombora manne yalitumiwa kutekeleza shambulizi hilo.

“Tumeona watu watatu wakiwemo watoto wawili waliokufa na wengine watano waliokuwa wamejeruhiwa akiwemo mwanamke mmoja,” alisema Ahmed.

Shambulizi hilo lilitekelezwa baada ya ikulu kuandaa sherehe ya kumpa mamlaka Rais Mohamed Abdullahi Farmajo kutoka kwa aliyekuwa kiongozi Hassan Sheikh Mohamud.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lilikiri kuhusika katika mashambulizi hayo kupitia kwa radio inayowaunga mkono, Radio Andalus.

Imekusanywa na BERNADINE MUTANU