http://www.swahilihub.com/image/view/-/4146314/medRes/1785106/-/fblbhyz/-/theresa.jpg

 

Theresa May kukutana na wapinzani Uingereza

Theresa May

Waziri Mkuu wa Uingereza Bi Theresa May aenda kuhudhuria kikao cha maswali katika bunge la wajumbe wa kawaida 'House of Commons' Oktoba 18, 2017 jijini London. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Friday, January 18  2019 at  13:38

Kwa Muhtasari

·      Waziri Mkuu wa Uingereza anakabiliwa na wakati mgumu kwani alitegemea Bunge litamuunga mkono kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya maarufu Brexit lakini wabunge wengi wamepinga uamuzi huo

 

·      Tayari kura nyingine ya uamuzi huo wa kujitoa Umoja wa Ulaya imepangwa Januari 29, 2019

 

LONDON, Uingereza

BAADA ya mpango wake wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya kukataliwa bungeni na yeye pia kunusurika kwenye kura ya kutokuwa na imani naye, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May sasa anajaribu kuwashirikisha wapinzani.

May anayekabiliwa na shinikizo kubwa, alikubali kuwa makubaliano aliyoyafikia na Umoja wa Ulaya, yamekataliwa, baada ya Serikali yake kupata pigo kubwa la kihistoria katika taifa hilo.

May na waliounga mkono mpango wake, walipata kura 202 pekee huku walioupinga wakipata kura 432 bungeni.

Huku muda ukizidi kwenda mbio, May aliwatolea wito viongozi wa upinzani kukutana naye kwa mazungumzo ya pamoja ya vyama vyote vya kisiasa, kabla ya kuwasilisha pendekezo mbadala kwa Bunge la nchi hiyo Jumatatu wiki ijayo.

“Makubaliano niliyoafikiana na UN yalikataliwa na wabunge, tena kwa kiasi kikubwa. Ninaamini ni wajibu wangu kutimiza takwa la Waingereza kujiondoa katika umoja huo na ninanuia kufanya hilo. Kwa vile wabunge wameweka wazi kile wasichokitaka, ni lazima tushirikiane pamoja kupata kile Bunge linachotaka,” alisema.

Lakini wapinzani wake waliwasilisha orodha ya matakwa yao ili kuwezesha ushirikiano na May, ikiwemo kufuta uwezekano kwamba Uingereza itaweza kujiondoa katika umoja huo mwezi Machi bila ya makubaliano kabisa.

Corbyn

May alisema kwamba alisikitishwa na uamuzi wa kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbyn kukataa kushiriki katika mashauriano naye. Hata hivyo May alisema milango bado iko wazi kwa yeyote kushiriki.

Mwenyekiti wa Chama cha Kihafidhina cha kiongozi huyo Brandon Lewis alisema kufuatia hali ya sasa ya Uingereza, kuwa nchi hiyo haiwezi kuwa katika umoja wa forodha na Jumuiya ya Ulaya kwa sababu kusaini mikataba ya biashara baada ya Brexit ni suala linalopewa kipaumbele.

Wakati majadiliano hayo yakijiri, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya pia zinajadiliana kuhusu namna ya kusonga mbele baada ya Bunge la Uingereza kuyakataa makubaliano ya May kuhusu Brexit.

Uingereza inatarajiwa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya ifikapo Machi 29, 2019.