'Trump Jr alikutana na maafisa wakuu wa Trump na afisa wa kijasusi'

Trump Junior

Trump Junior ni mwanawe Rais Donald Trump wa Marekani. Picha/HISANI 

Na SAMMY WAWERU na MASHIRIKA

Imepakiwa - Saturday, July 15  2017 at  17:58

Kwa Mukhtasari

Imefichuka kuwa mwana wa kiume wa Rais wa Marekani Donald Trump, Trump Jr mwaka 2016 alihudhuria mkutano wa maafisa wakuu wa Trump na aliyekuwa afisa wa kijasusi wa Urusi Rinat Akhmetshin katika jumba la Trump Tower.

 

IMEFICHUKA kuwa mwana wa kiume wa Rais wa Marekani Donald Trump, Trump Jr mwaka 2016 alihudhuria mkutano wa maafisa wakuu wa Trump na aliyekuwa afisa wa kijasusi wa Urusi Rinat Akhmetshin katika jumba la Trump Tower.

Aidha Rinat ambaye kwa sasa ni mkereketwa Jumamosi alithibitisha kwa vyombo vya habari vya Marekani kwamba alikuwa katika mkutano huo uliofanyika katika makao makuu ya Trump katika jumba la Trump Tower, Marekani.

Trump Jr aliahidiwa kupewa habari mbaya ili kumchafulia jina mpinzani mkuu wa babake wa chama cha Democrat Hillary Clinton katika mkutano huo, kwa mujibu wa baruapepe zake.

Mnamo Jumatano, Julai 12, 2017 alisema kuwa hakumfahamisha babake kuhusu mkutano wake na wakili raia wa Urusi Natalaia Veselnitskaya ambaye alisema kuwa angesaidia katika kampeni yake ya uchaguzi.

"Mkutano huo haukuhusu chochote kwa Hillary Clinton," Trump Jr akaambia kituo cha habari cha Fox News.

Aidha alitoa barua pepe zake zikionyesha kuwa alikaribisha ombi la kukutana na wakili huyo ambaye alikuwa na uhusiano na Urusi na aliyekuwa na ujumbe potovu kumhusu Hillary Clinton.

Awali alikuwa amekanusha kuwepo kwa mkutano uliofanyika Juni 9, 2016 kabla ya kubainika wiki hii.

Hata hivyo kamati ya haki ya bunge la seneti imemtaka Trump Jr kutoa ushahidi hadharani. Majopo kadhaa ya bunge la Congress nchini humo pamoja na majasusi wanachunguza madai kuwa Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani mwaka uliopita ili kumsaidia Donald Trump kuibuka mshindi.

Kwingineko, mwanamume mmoja aliyekuwa na kisu Jumamosi ameripotiwa kushambulia watalii wa kigeni nchini Misri katika ufuo wa mkahawa mkuu ulio katika ufuo wa Bahari ya Shamu ya Hurghada.

"Watu wawili wameuawa katika shambulio hilo ambapo watalii wengine wanne wamejeruhiwa vibaya," wakasema maafisa wa serikali na matabibu.

Hata hivyo mshambulizi huyo ametiwa mbaroni.

"Mshukiwa huyo anaendelea kuhojiwa ili tujue hasa lengo lake," wakaongeza maafisa wa Serikali ya Misri.

Aidha Wizara ya Usalama wa Ndani imedokeza kuwa mtu huyo aliogelea hadi walikokuwa watalii kutoka ufuo uliokuwa karibu.

Itakumbukwa kwamba mwaka 2016 kulikuwa na shambulizi jingine Hurgada lililopelekea watalii wawili kujeruhiwa.