Urafiki wa Bush, Michelle moto

George W. Bush akisalimiana na mke wa Obama, Michelle Obama wakati wa misa ya kumuaga rais wa zamani wa Marekani, George H.W Bush juzi mjini Washington   

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  09:10

Kwa Muhtasari

Alifunzwa kila mmoja anapaswa kuishi maisha ya heshima, ucheshi na ukarimu

 

 

Washington, Marekania. Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush ameendelea kudhihirisha ukarimu wake kwa familia ya Barack Obama wakati viongozi hao walipokutana kwenye misa ya kumuaga rais wa zamani George H.W Bush huku Bush mdogo akionekana kumpatia Michelle Obama peremende.

Tukio hilo lilitokea wakati Bush akiwa ameambatana na mkewe, Barbara wakiingia kanisani na alipofika sehemu walipokuwa wameketi marais wa zamani na wake zao, Bush alisalimiana nao na alimpomkaribia mke wa Obama, Michelle alisaliana naye na kisha akampatia peremende.

Hii ni mara ya pili kwa Bush kufanya tukio kama hilo na mara ya kwanza alionekana akimpatia Michelle ‘big g’ wakati walipokutana kwenye misa ya kumuaga seneta wa zamani wa Arizona, John McCain Septemba, 2018.

Baada ya kupokea peremende hiyo Michelle alionekana akitabasa huku Bush akiendelea kusalimiana na viongozi wengine waliohudhuria misa hiyo.

Misa hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Kathedro mjini Washington ilihudhuriwa na Rais Donald Trump pamoja marais wengine wa zamani Barack Obama, Bill Clinton, Jimmy Carter na George W. Bush.

Wawakilishi kutoka nje walikuwa ni pamoja na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa zamani wa Poland Lech Walesa na mwanamfalme wa Uingereza Charles.

Tukio hilo lilionekana na wengi kama njia bora ya kumuaga rais huyo wa zamani aliyetajwa kuwa ni mzalendo aliyehusika katika kuungana kwa amani Ujerumani na kumalizika kwa Vita Baridi.

George W. Bush alisoma historia ya maisha ya babake akisema alimfunza kila mmoja kuishi maisha ya heshima, ucheshi na ukarimu. Hata hivyo, rais huyo wa zamani alishindwa kujizuia na kujikuta akimwaga machozi wakati akimwelezea babake. Baadaye alifuta machozi na kuendelea na hotuba yake na baada ya muda alimaliza na kuondoka jukwaani.

Wakati akirejea sehemu yake aligusa jeneza lilikuwa na mwili wa babake na alikwenda kuketi alionekana bado akibubujikwa na machozi hali iliyomfanya kaka yake, Jeb Bush kumfariji.