Uswizi kurejesha Kenya fedha zilitumwa kwa njia ya magendo

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akiteta jambo na Rais wa Uswisi, Alain Berset baada ya kutia saini ya makubaliano ya kurejesha fedha nchini Kenya  

Imepakiwa - Wednesday, July 11  2018 at  09:12

Kwa Mukhtasari

Pande hizo zimedhamiria kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia

 

Nairobi, Kenya. Wananchi wa Kenya wameanza kufufua matumaini yao juu ya kurejeshwa nyumbani mamilioni ya fedha yaliyotoroshwa nchini Uswisi kwa njia za kimagendo ikiwamo zile zilizopatikana kwa njia za kifisadi.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametia saini pamoja na mwenzake wa Uswisi, Alain Berset aliyeko nchini humo kwa ziara ya siku mbili. Viongozi hao pia walikubaliana kuendelea kupanua ushirikiano wa kibiashara na kuahidi kudumisha mikakati ya vita dhidi ya vitendo vya ufisadi.

Vongozi hao waliingia makubaliano kwamba Serikali ya Uswizi itarejesha fedha zinazofungamana na uhalifu na ufisadi na ambazo zinaendelea kuhifadhiwa katika benki za taifa hilo la Ulaya.

Wawili hao aidha walikubaliana kwamba Kenya itafungua ubalozi mpya katika jiji la nchi hiyo, Bern ikiwa ni ishara nyingine inayotoa matumaini kuwa pande hizo mbili zimedhamiria kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.

Kutokana na hatua hiyo wananchi wengi wa Kenya wamekuwa wakielezea matumaini kuhusiana na kurejeshwa kwa fedha hizo haraka iwezekanavyo.

Wakati hali ikiwa hivyo nchini Kenya, nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inaaarifiwa kuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila amesema hatakutana wala kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley ambaye anatazamiwa kuitembelea nchi hiyo wiki hii.

Msemaji wa serikali ya DRC amesema, Lambert Mende ameondoa uwezekano wa Rais Kabila kukutana na mwanadiplomasia huyo.

“Kuhusu Nikki Haley, nashangaa kwa nini hatua ya Rais Kabila kukataa kuonana naye linaonekana kama suala la utata. Balozi huyo wa Marekani alikuwa hapa Kinshasa mwezi Oktoba mwaka jana na wakafanya mazungumzo na Rais Kabila kwa takriban dakika 90, “ alisema.

Haijabainika iwapo mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa atalazimika kufuta safari yake hiyo ya kuitembelea Congo au la.

Kadhalika serikali ya Rais Kabila imeahirisha safari iliyotazamiwa kufanyika wiki hii ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.