http://www.swahilihub.com/image/view/-/4759634/medRes/2109845/-/144r1bnz/-/spika.jpg

 

Vyombo vya habari vyatakiwa kuwajibikia

Spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  16:34

Kwa Muhtasari

Vyombo vya habari ni nguzo muhimu kwa serikali na taifa kwa jumla

 

Mombasa, Kenya. Vyombo vya habari, watangazaji na waandishi wake wametakiwa kuwajibika kazini.

Wabunge kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari Ijumaa mjini Mombasa, wameitaka taasisi hii muhimu kuwa na ukweli na usawa kwenye utendakazi wake hasa inaporipoti.

Spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi alisema wabunge wanatambua juhudi za vyombo vya habari ingawa vinafaa kumakinika. "Vyombo vya habari ni nguzo muhimu kwa serikali na taifa kwa jumla, tunaomba muendelee kwa kazi hiyo kuntu na bora japo uwajibikaji uwepo," akasema Bw Muturi.

Kiongozi wa wachache bungeni, na ambaye ni mbunge wa Suba Kusini John Mbadi alisema haja ipo kwa vyombo vya habari kuripoti mambo kikamilifu pasi kuongeza chuku. "Sisi kama wabunge tunaomba vyombo vya habari na waandishi wake waripoti mambo yalivyo kwa njia ya ukweli na usawa," akasema.

Akirejelea majukumu ya wabunge, Mbadi alisema mwandishi anaporipoti jinsi mbunge anahusishwa na sakata za ufisadi, mhariri anafaa kuwa na ushahidi wa kutosha kuruhusu habari hiyo kwenda hewani ama kuchapishwa magazetini, na kwenye mitandao ya kijamii. Aliteta kuwa wabunge wengi wamepakwa tope kwa sababu ya visa ambavyo hawahusishwi navyo.

Mwenyekiti huyo wa Orange Democratic Movement (ODM) alipendekeza ripota anapofichua kashfa zinazowazunguka wabunge, chombo husika cha habari kinafaa kumruhusu afike mbele ya kikao cha faragha cha wabunge ili kutoa ushahidi wake. "Mwandishi anaporipoti kisa cha ufisadi kinachomhusu mbunge ama wabunge, tunaomba awe akifika mbele ya kikao faragha cha wabunge ili kutoa ushahidi wake," akasema.

Wabunge wamekuwa mstari wa mbele kutetea uhuru wa vyombo vya habari nchini. Mbadi hata hivyo, anavitaka viwe vikijidhibiti kwa majukumu yake na kuwajibika kikamilifu.

Alisema amepokea visa kadha kutoka kwa waandishi wa habari wakilalamika kwamba wahariri hubadilisha ukweli uliopo kwenye habari ili kuegemea upande wanaotoka. Vyombo vya habari, watangazaji na waandishi wake ndio 'macho, maskio na mdomo wa umma', ambapo huwa katika mstari wa mbele kutetea raia.

Visa vingi vya ufujaji wa mali ya umma, ufisadi, matumizi mabaya ya mamlaka na ofisi hufichuliwa na vyombo vya habari. Ni taasisi ambayo imevalia njuga kutetea haki za kibinadamu, mbali na mashirika husika. Pia, vyombo vya habari vimesaidia kuinua kimaisha ya baadhi ya watu kwa kuangazia ulemavu, shida ama juhudi zao.

Hata hivyo, waandishi wa habari wakati mwingine  huandamwa na serikali, baadhi ya watu mashuhuri hasa wanaohusishwa na maovu, na hata maafisa wa polisi. Kuna wanahabari kadha ambao wamejeruhiwa na wengine kuuawa wakati wakitekeleza majukumu yao.