Wajumbe UN walumbana kuhusu Somalia

Naibu msemaji wa UN, Farhan Haq   

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  09:25

Kwa Muhtasari

Balozi atahadharisha huenda makundi ya kigaidi yakaongezeka

 

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa (UN) aliyeamriwa kuondoka nchini Somalia amesema taifa hilo linakabiliwa na machafuko ya kisiasa huku balozi wa Somalia akilitaka Baraza la Usalama kuacha kuingilia mambo ya ndani ya nchi yake.

Wakizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama UN, wiki iliyopita, wanadiplomasia hao walitoa kauli zinazohitilafiana, baada ya Somalia kumuamuru Nicholas Haysom kuondoka nchini humo, ikimtuhumu kukiuka mipaka ya kazi yake.

Haysom aliliambia Baraza hilo kwamba hali ya kisiasa nchini Somalia inatishia kulitumbukiza tena taifa hilo kwenye machafuko makubwa.

Mjumbe huyo wa UN alifukuzwa baada ya kuhoji kukamatwa kwa watu kadhaa, akiwemo Mukhtar Robow, kiongozi wa zamani wa kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Balozi wa Somalia kwenye Umoja wa Mataifa aliliambia Baraza la Usalama kwamba licha ya nchi yake kushukuru kwa msaada wa umoja huo, lakini ina haki ya kuheshimiwa masuala yake ya ndani.

Naibu msemaji Farhan Haq amesema jumuiya hiyo ya kimataifa bado inatafuta ufafanuzi zaidi juu ya jambo hilo, lakini Balozi Haysom anaendelea kuungwa mkono na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres.

Haysom mwenyewe hazungumzii moja kwa moja kufukuzwa kwake lakini wakati anaposifia maendeleo ya Somalia katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na mipango ya usalama, alisema mivutano ya kisiasa inayoendelea nchini Somalia inaweza kuitumbukiza nchi hiyo kwenye matatizo, akitolea mfano wa kukamatwa kwa Mukhtar Robow na nguvu zilizotumika.

Alisema maandamano yaliyofuatia baada ya kukamatwa Robow si mfano mzuri kwa uchaguzi ujao. Mwanadiplomasia huyo aliongeza kusema kwamba hatua hiyo inaweza kuchochea uwezekano wa kurudi kwenye makundi yenye msimamo mkali watu waliojitoa kwenye makundi hayo kwa kuzingatia kuacha vurugu kwa ajili ya kutekeleza mabadiliko ya kisiasa.