Walionasa pangoni kwa siku 18 waokolewa wote wakiwa hai

Askari wakiwa pangoni katika operesheni ya mwisho ya uokoaji. Picha na AFP 

Imepakiwa - Wednesday, July 11  2018 at  09:34

Kwa Muhtasari

Awamu tatu za uokoaji zilifanikiwa kwa muda usiopungua saa 35

 

Thailand. Kama ni sinema basi inafaa kusema picha limekamilika na mwongoza picha ameibuka shujaa baada ya kumaliza kuruka viunzi vyote ikiwamo vile vilivyotazamwa kama ni hatari kwa maisha.

Timu ya waokoaji walioendesha operesheni ya kuwaokoa vijana 12 pamoja na mwalimu wao waliokuwa wamenasa pangoni, Kaskazini mwa Thailand sasa wana kila sababu ya kushusha chini pumzi na pengine kujipongeza angalau kwa glasi ya mvinyo baada ya kufanikiwa kuwaokoa wote tena wakiwa salama.

Ilikuwa kazi iliyohitaji tahadhari na moyo wa kujituma kutembea umbali wa kilometa 800 ndani ya pango na kisha kuwafikia vijana hao waliosota pangoni humo kwa siku 18. Operesheni ya kwanza iliyoanza kuzaa matunda ilifanyika Jumapili huku kundi la kwanza la watoto wanne wakiondolewa kwenye kadhia hiyo. Kisha kazi hiyo ilirudiwa siku iliyofuata ikishuhudiwa watoto wengine wanne wakiokolewa.

Ili kufanikisha mkakati huo, waokoaji 900 wa ndani na nje ya Thailand waliopangika makundi walijikusanya pamoja na kuratibu safari ya kuwafuata watoto hao walioingia kwenye pango hilo kwa shughuli za michezo na kitalii. Ingawa kazi ya uokoaji ilikabiliwa na changamoto nyingi, wataalamu waliandaa michoro pamoja na vifaa vingine vya msaada wa hewa ya oksijeni walivyotumia wakati wote wa operesheni.

Waokoaji hao walitumia muda wa saa 11 kukamilisha operesheni moja ingawa katika siku ya mwisho walifanikiwa kuokoa watano katika operesheni ambayo ilitumia muda mwingi zaidi. Awamu zote tatu za uokoaji zilifanikiwa kwa muda usiopungua saa 35. Watoto hao walinasa kwenye pango hilo Juni 23 wakati walipokuwa katika safari ya utalii. Walitarajiwa kuwa miongoni mwa watoto watakaoalikwa na Shirika la Soka Duniani (FIFA) kuhudhuria Fainali za Kombe la Dunia zinazofanyika Urusi.

FIFA ilisema jana kuwa kuna uwezekano mdogo watoto hao wakaalikwa kuhudhuria mchezo wa mwisho wa fainali kutokana na kuhitaji muda zaidi kuchunguzwa afya zao. Baadhi yao imedaiwa wameanza kutibiwa matatizo ya mapafu na homa ya nimonia.

Timu ya waokoaji ilisema jana ilikuwa siku ambayo ingefanikiwa kuwaondoa watu wote walionasa kwenye pango hilo na suala hilo lilipewa msukumo zaidi kutokana utabiri wa hali ya hewa kuonyesha uwezekano wa kutokea mvua kubwa zaidi kuanzia leo.

Watoto hao katika kipindi chote tangu wagundulike kunasa kwenye pango hilo, walikuwa wakiangaliwa kwa karibu na daktari mmoja na wapigambizi watatu kutoka kikosi cha askari wa wanamaji waliokuwa pangoni humo wakiendelea kufanya uangalizi wa maisha ya vijana hao. Walitarajiwa kuondoka wakati vijana hao watakakapookolewa.

Kwa mujibu wa maofisa wa afya, wavulana wanane waliookolewa ndani ya siku mbili zilizopita wanasemekana kuwa katika ‘ari kubwa’ na wana kinga imara kwasababu ni wachezaji wa mpira. Madaktari wamekuwa na tahadhari kwa sababu ya hatari ya kupata maambukizi na wamewatenga watoto hao hospitali.

Gavana wa Chiang Rai, Narongsak Osatanakorn amesema kwamba operesheni ya kuwaokoa Jumanne ilianza saa 10 alfajiri ikihusisha wapiga mbizi 19. Timu ya madaktari na wanajeshi wanamaji watatu wa Thailand ambao walikaa na wavulana hao katika eneo dogo kavu ndani ya pango nao watatoka.

“Tunatarajia kama hakuna kitakachozuia, ninathibitisha kwamba watoto wanne, kocha mmoja, madaktari na maafisa watatu wanamaji ambao walikuwa na watoto tangu siku ya kwanza walipowapata, watatoka nje ya pango,” alisema.

Gavana huyo alisema operesheni ya jana ingechukua muda mrefu tofauti na zilizopita ambazo zilitumia saa 11. Hali ya wavulana hao na kocha wao imevuta hisia za wananchi wa Thailand na duniani kote, kutoka taarifa ya kupotea kwao hadi kutolewa kwa mkanda wa video wa kwanza ulioonyesha kuwa wamepatikana na wako hai siku 10 baadaye na wapiga mbizi wa kutoka Uingereza.