http://www.swahilihub.com/image/view/-/4928678/medRes/2220022/-/8njo06z/-/felix.jpg

 

Wapinzani wadai ushindi wao DRC

Felix Tshisekedi (mwenye shati jeupe mbele) akiwa pamoja na wafuasi wake 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  09:43

Kwa Muhtasari

Wanasiasa wa upinzani waituhumu Serikali kutaka kuiba kura.

 

Kinshasa, DRC. Timu ya kampeni ya mgombea urais Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC), Felix Tshisekedi, imesema wawakilishi wa kambi yao wamekutana na kambi ya Rais anayemaliza muda wake, Joseph Kabila kuhakikisha makabidhiano ya amani ya madaraka.

Kambi ya Kabila hata hivyo imekanusha kuwepo na mikutano kama hiyo tangu kufanyika kwa uchaguzi wa Desemba 30, ambao matokeo yake ya awali yanatarajiwa kutangazwa wiki hii.

Uchaguzi huo ulitarajiwa kuleta mabadiliko ya kwanza ya Kidemokrasia nchini humo katika kipindi cha miaka 59 ya uhuru wake, lakini wasiwasi unazidi kuenea huku baadhi ya wanasiasa wa upinzani wakiituhumu Serikali kutaka kuiba kura.

Matokeo yanayobishaniwa huenda yakazusha aina ya vurugu zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi wa mwaka 2006 na 2011 na kuvuruga tena usalama katika maeneo ya mpakani mwa DRC na Uganda, Rwanda na Burundi.

Tshisekedi aligombea urais akichuna na mgombea aliyeteuliwa na Kabila mwenyewe Emmanuel Shadary, na kiongozi mwingine wa upinzani Martin Fayulu, ambaye uchunguzi wa maoni ya wapigakura kabla ya uchaguzi ulimuonyesha akiongoza kinyang’anyiro hicho.

Wafuasi wa Fayulu

Ripoti za mawasiliano kati ya kambi za Tshisekedi na Kabila zimewapa wasiwasi baadhi ya wafuasi wa Fayulu wakihofia kwamba huenda Kabila anajaribu kujadili ugawanaji wa madaraka na Tshisekedi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Tshisekedi cha UDPS, alisema mawasiliano kati ya kambi mbili hizo yalikuwa yanachangia maridhiano ya kitaifa, na kwamba chama cha UDPS kinapinga sera yoyote ya kulipiza visasi.

“Watu hao wawili (Kabila na Tshisekedi) wana maslahi katika kukutana kuandaa mazingira ya amani na ya ustaarabu ya kukabidhiana madaraka,” Jean-Marc Kabund alisema.

Msemaji wa Tshisekedi, Vidiye Tshimanga, alisema Kabila na Tshisekedi hawajakutana ana kwa ana tangu uchaguzi lakini wawakilishi wake wamekutana mara kadhaa.

Kambi ya Kabila yakana

Mmoja wa washauri wa Kabila na msemaji wa Shadary, Barnabe Karubi alikanusha kuwapo kwa mawasiliano yoyote na Tshisekedi au wawakilishi wake.

Alisema muungano wa vyama tawala umeituhumu kampeni ya Fayulu na maaskofu wa Congo kwa kujaribu kuchochea vurugu za baada ya uchaguzi katika taifa hilo kubwa lenye utajiri wa madini.

Wiki iliyopita, maaskofu nchini humo walisema wanajua mshindi wa uchaguzi, tangazo lililotafsiriwa na wengi kama onyo kwa mamlaka dhidi ya wizi wa kura.

Kasoro zajitokeza

Ujumbe wa uangalizi wa uchaguzi ulidai kushuhudia kasoro 52 katika vituo 101 vya kuhesabu kura ulikotuma waangalizi, ikiwa ni pamoja na watu kuchezea matokeo.

Ripoti ya Shirika la SYMOCEL lenye makao yake nchini DRC ilisema asilimia 16 ya vituo vya kuhesabu kura vilitegemea matokeo kutoka kwenye mashine badala ya kura zilizohesabiwa kwa mkono.