http://www.swahilihub.com/image/view/-/4800820/medRes/2135201/-/14tcdvsz/-/nene.jpg

 

Waziri wa Fedha ajiuzulu kwa kashfa, mwingine aapishwa chapuchapu

Waziri wa Fedha, Nhlanhla Nene  

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  08:49

Kwa Muhtasari

Alijikuta akigubikwa katika kashfa kuhusu vikao vya siri

 

 

Johannesburg, Afrika Kusini. Rais Cyril Ramaphosa Jumanne aliridhia kujiuzulu kwa Waziri wa Fedha Nhlanhla Nene, ambaye alijikuta akigubikwa katika kashfa kuhusu vikao vya siri alivyokuwa amefanya kati ya mwaka 2010 na 2013 na familia tata ya akina Gupta.

Mbali ya kuridhia, Ramaphosa alimteua Tito Mboweni, gavana wa zamani wa Benki ya Akiba, na aliapishwa chapuchapu ili aweze kuanza majukumu yake mapya.

Nene amekuwa akipokea simu zinazomshinikiza kujiuzulu baada ya kukiri kuwa aliwahi kuitembelea familia ya akina Gupta, marafiki wa rais wa zamani aliyezingirwa na kashfa Jacob Zuma akishutumiwa kwa kushindwa kufichua vikao hivyo mapema.

Zuma na familia ya akina Gupta wamekana kutenda kosa.

“Ni baada ya kujipima mwenendo wake na dhamira kwa nchi yake kwamba ameamua kujiuzulu si kwamba amehusishwa kutenda kosa,” alisema Ramaphosa Jumanne.

Upinzani

Makundi ya upinzani katika Afrika Kusini vikiwemo vyama vya Democratic Alliance (DA) na Economic Freedom Fighters (EFF) yamekuwa yakitoa wito kwa Nene kujiuzulu.