http://www.swahilihub.com/image/view/-/4706172/medRes/2074761/-/jocnym/-/biti.jpg

 

Waziri wa Zimbwabwe anyimwa hifadhi Zambia

Kiongozi wa Muungano wa Upinzani nchini Zimbabwe MDC, Tendai Biti  

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  09:07

Kwa Muhtasari

Alichochea ghasia katika uchaguzi na kukimbilia Zambia

 

Harare, Zimbabwe. Kiongozi wa Muungano wa Upinzani nchini Zimbabwe MDC, Tendai Biti amenyimwa hifadhi nchini Zambia.

Polisi wa Zimbabwe wanamlaumu Biti kwa kuchochea ghasia kufuatia uchaguzi wa wiki iliyopita kisha kukimbilia Zambia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia, Joe Malanji aliliambia Shirika la Habari la Uingereza (BBC) kuwa sababu za Biti kuomba hifadhi zilikuwa dhaifu. “Alizuiwa eneo salama hadi pale aliporejeshwa Zimbabwe,” alisema waziri huyo.

Ripoti nyingine za polisi wa Zambia zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinasema kuwa maofisa wa Zimbabwe walijaribu kumkamata mwanasiasa huyo baada ya kuvuka mpaka na kuingia Zambia.

Taarifa zilisema kwamba mwanasiasa huyo aliomba msaada kwa sauti huku watu waliokuwa wakisafiri zaidi ya watu 300 wa Zimbabwe waliwazuia maofisa usalama wa Serikali kumkamata.

Maofisa wa Zambia waliingilia kati na kutishia kuwakamata maofisa wa Zimbabwe kwa kujaribu kutekeleza wajibu wao ndani ya ardhi ya Taifa hilo jirani.

Kulikuwa na matumaini kuwa uchaguzi wa Julai nchini Zimbabwe ungeleta mabadiliko makubwa baada ya kumalizika kwa utawala wa Robert Mugabe.

Hata hivyo wiki iliyopita watu sita waliuawa baada ya jeshi kuingilia kati kuzima maandamano ya upinzani kwenye mji mkuu wa Harare. Waandishi wa habari walisema kuna hofu nchini humo huku baadhi ya wanachama wa upinzani wakikimbilia mafichoni.

Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Rais Emmerson Mnangagwa kushinda uchaguzi, lakini muungano wa MDC unadai uchaguzi haukuwa wa haki.

Upinzani unasema mgombea wake, Nelson Chamisa ndiye alikuwa mshindi. Biti alikuwa waziri wa Fedha kwenye Serikali ya umoja wa kitaifa iliyobuniwa baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata wa mwaka 2008 na ilisifiwa kwa kusaidia kuboresha uchumi.

Wakili wa upinzani, Thabani Mpofu alisema wameandaa ushahidi kuonyesha kura zilivyoibwa.