http://www.swahilihub.com/image/view/-/4369432/medRes/1927415/-/i3usdkz/-/madikizela.jpg

 

Winnie Madikizela-Mandela azikwa nchini Afrika Kusini

Winnie Madikizela-Mandela

Picha ya Agosti 15, 1985, ya Winnie Madikizela-Mandela, wakati huo akiwa mke wa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela, alipokuwa amemtembelea mumewe aliyekuwa amefungwa katika gereza la Johannesburg. Winnie Mandela alifariki akiwa na umri wa miaka 81 Aprili 2, 2018, katika hospitali ya Johannesburg baada ya kuugua kwa muda mrefu, kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wake Victor Dlamini. Picha/AFP 

Na AFP

Imepakiwa - Saturday, April 14  2018 at  12:31

Kwa Muhtasari

Marehemu Winnie Madikizela-Mandela ambaye alikuwa mke wa zamani wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela, anapewa mazishi ya kishujaa jijini Johnesburg nchini humo.

 

SOWETO, Afrika Kusini

MAREHEMU Winnie Madikizela-Mandela ambaye alikuwa mke wa zamani wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela, anapewa mazishi ya kishujaa jijini Johnesburg nchini humo.

Hafla hiyo ya aina yake ilihudhuriwa na maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya Afrika Kusini.
Kabla ya mazishi hayo ibada ya kufana iliandaliwa katika uwanja wa michezo wa Orlando mjini Soweto na kuhudhuriwa na maelfu ya waombolezaji wakiongozwa na Rais Cyril Ramaphosa.

Wanajeshi wa Afrika Kusini wamefyatua risasi 21 kabla ya wanajeshi kusindikiza maiti yake hadi bustani ya Four Way Memorial kwa mazishi.

Sherehe hizo zinafika kilele chake baada ya siku 10 za maombolezo ya kitaifa nchini Afrika Kusini ambapo maelfu ya raia walitoa heshima zao za mwisho kwa marehemu ambaye alijulikana kama, “Mama wa Taifa”.

Winnie Mandela ambaye alifariki mnamo Aprili 2, 2018, jijini Johannesburg baada ya kuugua kwa muda mrefu alipambana vikali na utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Aliendeleza mapambano hayo hata baada ya shujaa Nelson Mandela kusukumwa gerezani kwa miaka 27.

Awali, mwili wa Winnie Mandela ulisafirishwa kutoka hifadhi ya miti hadi nyumbani kwake mjini Soweto.

Mamia ya watu walijitokeza kwenye barabara za mji huo huku gari lililobeba jeneza lenye mwili wake likisindikizwa na wanajeshi waliokuwa wamebeba bendera ya chama tawala, African National Congress (ANC). Jeneza hilo pia lilifunikwa kwa bendera ya ANC.

Rais Ramaphosa pia amewaangoza wambolezaji katika ibada ya wafu ambayo pia ilihudhuriwa na marais wa Namibia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Vilevile, alikuwepo waziri mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga amehudhuria hafla ya mazishi.

Mwanaharakati wa haki za raia nchini Marekani Jesses Jackson pia amehudhuria mazishi hayo.

“Kweli yeye ni mama wa Afrika Kusini,” Jackson aliwaambia wanahabari Ijumaa.