http://www.swahilihub.com/image/view/-/4938064/medRes/1240799/-/bwc9ae/-/630382-01-02.jpg

 

Baada ya miaka saba ICC yamwachia huru Gbagbo

Laurent Gbagbo

Aliyekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Wednesday, January 16  2019 at  17:26

Kwa Muhtasari

Kiongozi huyo wa zamani wa Taifa la Ivory Coast aliachiwa huru baada ya kubainika kwamba hana kosa lolote ambalo alilifanya wakati wa utawala wake.

 

YAMOUSSOUKRO, Ivory Coast

MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), imemwachia huru rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake.

Rais huyo mstaafu wa Taifa la Ivory Coast, Gbagbo alishtakiwa kwa madai ya kuhusika na vurugu zilizosababisha mauaji ya watu 3,000 huku wengine 500,000 wakiyakimbia makazi yao

Gbagbo alifikishwa mbele ya mahakama hiyo mwaka 2011 kutokana na vurugu za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010 ambao ulishuhudia akishindwa mbele ya mpinzani wake, Alassane Ouattara.

Katika uamuzi wao, majaji wa ICC, waliamuru Gbagbo kuachiwa huru kwa kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha shtaka hata moja kati ya yale aliyoshitakiwa mbele ya mahakama hiyo.

Gbagbo alishitakiwa kwa madai ya kuhusika na vurugu zilizosababisha mauaji ya watu 3,000 huku wengine 500,000 wakiyakimbia makazi yao.

Kwa mujibu wa rekodi za ICC, Gbagbo ni kiongozi mkuu wa kwanza wa zamani wa nchi kupandishwa mbele ya mahakama hiyo. Kukamatwa kwake kulitekelezwa na vikosi vilivyokuwa vikiungwa mkono na Umoja wa Mataifa (UN) na Ufaransa. Mbali na Gbagbo, mke wake Simone Gbagbo, naye alitiwa hatiani na mahakama za nchi hiyo kwa kuhusika na makosa mbalimbali ikiwemo kuratibu makundi ya ujambazi.

Serikali ya Ivory Coast ilikataa kumkabidhi Simone kwa ICC ikisema itamshitaki na kumhukumu katika mahakama za ndani.

Alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mbalimbali ikiwamo ya uvunjifu wa sheria za nchi, kuvuruga usalama wa nchi na makosa dhidi ya ubinadamu.

Simone alinufaika na msamaha wa Rais Ouattara mwaka jana ambaye alisema alimsamehe ili kufungua milango ya majadiliano na maridhiano kwa mustakbali wa taifa hilo linaloongoza kwa kilimo cha kakao duniani.

'Hana kesi ya kujibu'

Majaji wa Mahakama ya ICC walisema kiongozi huyo wa zamani hakuwa na kesi ya kujibu kwa kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.

Jaji Cuno Terfusser aliyekuwa akiendesha kesi hiyo alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kwamba hotuba za Gbagbo zilihusisha au kuamrisha madai ya uhalifu uliotendeka.

Wafuasi wa Gbagbo walisherehekea katika maeneo mbalimbali baada ya hukumu hiyo kutoka mahakamani.

Hata hivyo watu wasiopungua 200 walioathirika na machafuko hayo walifika kwenye mji wa Abidjan jana kuitaka Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague isimuachie huru Gbagbo.