http://www.swahilihub.com/image/view/-/3881804/medRes/1609943/-/kgidrwz/-/trra.jpg

 

Bosi wa Freemasons aaga dunia

Jayantilal Keshavji

Marehemu Sir Jayantilal Keshavji “Andy Chande”. Picha/MAKTABA 

Na WAANDISHI WETU

Imepakiwa - Friday, April 7  2017 at  17:55

Kwa Muhtasari

Aliyekuwa kiongozi wa Jumuiya ya Freemasons Tanzania na Afrika Mashariki Sir Jayantilal Keshavji “Andy Chande” ameaga dunia.

 

ALIYEKUWA kiongozi wa Jumuiya ya Freemasons Tanzania na Afrika Mashariki Sir Jayantilal Keshavji “Andy Chande” ameaga dunia.

Sir Chande amekuwa mwanachama wa Freemasons kwa takriban miongo sita tangu ajiunge na umoja huo mwaka 1954.
Historia yake

Sir Chande alizaliwa Mombasa Kenya Mei 7, 1928 ingawa wazazi wake walikuwa wakiishi Bukene mkoani Tabora, magharibi mwa Tanzania.

Alifika Tanzania mwaka 1950 na alikutana na watu wengi ambao walikuwa wanahudhuria vikao vya Freemasons.

Wakati huo watu hawakuwa huru kuzungumzia Freemasons kama aliyofanya Sir Chande hasa kabla ya vita vikuu ya pili ya dunia.

Wakati huo Freemasons ilikuwa imegawanyika makundi tofauti katika shule, hospitali na mashirika.

Kundi maalumu lilikuwa ni la matajiri na wafanyakazi wakubwa serikalini, wakiwamo Wazungu na Wahindi.

Ilimchukua miaka miwili kukubaliwa kujiunga na Freemasons na aliapishwa rasmi mwaka 1954 akiwa na miaka 28.
Baada ya hapo alipewa nafasi ya kuongoza tawi la Freemasons katika nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi.

Sir Chande alistaafu kama kiongozi wa Freemasons Afrika Mashariki mwaka 2005 na aliendelea kushiriki mikutano huko Uingereza kwa sababu alikuwa akiendelea kufanya kazi na mashirika ya huko.

Ahojiwa na Kamati ya Moi Kenya

Katika miaka ya 1990 Freemasons ilipata changamoto kubwa nchini Kenya baada ya Rais Daniel Arap Moi kuunda tume ya kuchunguza watu wanaoabudu shetani ambayo moja ya majukumu ya tume yalikuwa ni kuichunguza Freemasons.

“Nilifika mbele ya tume mara mbili na katika nyakati tofauti kama Mkuu wa Freemasons Afrika Mashariki. Nilitoa ushahidi kuhusu kazi tunazifanya,” alikaririwa Sir Chande.

Ijapokuwa tume hiyo haikutoa majibu ya kazi waliyokabidhiwa na Rais Moi, inasemekana kuwa ilisafisha tuhuma zilizoelekezwa kwa Freemason.
“Nafurahi kusema kuwa tuhuma zile zilisafishwa zaidi na Rais aliyefuata baadaye Rais Mwai Kibaki ambaye katika moja ya hotuba zake alisema Freemasons imetoa mchango mkubwa sana nchini Kenya,” alisema Sir Chande.

Kazi zinazofanywa na Freemasons

Kazi zinazofanywa sasa hivi ni kuwafundisha wanachama wake kuhusu majukumu yao kwa Mwenyezi Mungu, kwa nchi zao, familia zao na nchi wanazofanyia kazi hata kama ni ugenini.

Jinsi ya kujiunga
Ili kujiunga na Freemasons ni lazima uwe na umri wa miaka 21. Ni hiari pia uwe unamwamini Mungu haijalishi ni Mungu gani na watu ambao hawamwamini Mungu hawaruhusiwi kuwa wanachama wa Freemasons na ni lazima uwe mkweli.

Pia ni lazima familia yako ikubali wewe kujiunga na Freemasons.

Ni lazima upeleke maombi yako kwa mtu unayemfahamu ambaye yuko Freemasons au kama humjui mtu unapawa kuandika barua na kamati itakupeleleza wewe na familia yako na pia watakutembelea nyumbani na kuongea na familia yako.

Inawezekana ikachukua mwaka mmoja hadi mwaka na nusu kuruhusiwa kujiunga.

Baada ya kujiunga

Unatakiwa kujifunza vitu vingi na kuvihifadhi kichwani kama vile maneno ya kusema wakati unafanya ibada za Freemasons kwa sababu unavyozungumzia sifa za kuwa binadamu kamili unaweza ukafananisha na ibada ya kanisani.

Faida

Hakuna faida za kupata fedha kama wengi wanavyoambiwa kwamba ukijiunga na Freemasons unapewa fedha nyingi.

Faida ni kuongeza idadi ya marafiki na kuongeza ufahamu.

Hakuna utoaji wa kafara kama inavyosemekana na pia hakuna uhusiano kati ya Freemasons na Agano la Kale.