http://www.swahilihub.com/image/view/-/4369558/medRes/1927568/-/12v66b9/-/tshisekedi.jpg

 

Hisia mseto Felix Tshisekedi akitangazwa mshindi wa urais DRC

Mwanawe Tshisekedi ateuliwa kuwania urais DRC

Felix Tshisekedi. Picha/MAKTABA 

Na AFP

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  12:59

Kwa Muhtasari

  • Ufaransa yasema ni matokeo ambayo haikutarajia
  • Ubelgiji yapanga suala hilo lijadiliwe kwa kina

 

KINSHASHA, DRC

MWAMKO mpya wa kisiasa jana ulishuhudiwa katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) baada ya Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo kumtangaza kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi kama mshindi wa kiti cha urais.

Ushindi huo wa kihistoria ulizua furaha riboribo kote nchini humo hii ikiwa mara ya kwanza baada ya miaka 18 ambapo Rais aliye mamlakani atamkabidhi hatamu ya uongozi kwa kiongozi wa upinzani kwa njia ya amani.

“Baada ya kujizolea asilimia 38.7 za kura. Felix Tshisekedi anatangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu na Rais mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo," akasema Corneille Nangaa, Mkuu wa Tume Huru ya Kitaifa ya uchaguzi nchini humo (CENI).

Hata hivyo, mwaniaji maarufu wa upinzani Martin Fayulu aliyemaliza wa pili aliyakataa matokeo hayo na kuyataja kama 'mapinduzi ya uchaguzi'. 

"Matokeo haya hayana ukweli kuhusu maamuzi ya wapiga kura. Haya ni mapinduzi ya kura," akasema Bw Fayulu bila kufafanua iwapo ataenda mahakamani kuyapinga kwa kuwa katiba ya nchi hiyo inamruhusu mwaniaji asiyeridhishwa na matokeo ya kura za urais kuelekea mahakama ya juu kuyapinga ndani ya muda usiozidi siku 14.

Kiongozi huyo alionyeshwa na kampuni mbalimbali zilizoandaa kura ya maoni kabla ya uchaguzi huo kama aliyekuwa mstari wa mbele kukitwaa kiti hicho. 

DRC imekuwa ikikumbwa na mzozo wa siasa za urithi kwa muda wa miaka miwili iliyopita baada ya Rais Joseph Kabila kutangaza mwaka jana kwamba hangewania wadhifa huo tena. Rais Kabila amekuwa mamlakani kwa muda wa miaka 18.

Shadary amaliza wa tatu

Mwaniaji wa chama tawala aliyekuwa akipigiwa debe na Rais Kabila, Ramazani Shadary aliibuka wa tatu katika uchaguzi huo. 

Kiujumla, Bw Tshisekedi alipokea zaidi ya kura milioni saba, Bw Fayulu akapata zaidi ya kura milioni sita naye Bw Ramazani akapata zaidi ya kura milioni nne.

Awali, kanisa Katoliki linalojivunia ufuasi mkubwa wa kidini nchini DRC ilisema kwamba inajua mshindi halisi wa kura hizo japo tume ya uchaguzi iliwazuia kutangaza mshindi wao. Hali hii huenda ikazua utata zaidi iwapo kanisa hilo litatangaza Bw Fayulu kama mshindi wa kura hiyo na kupinga tangazo la CENI.

Rais mteule Tshisekedi, 55 ni mwanawe aliyekuwa mwanasiasa mkongwe wa upinzani marehemu Étienne Tshisekedi aliyefariki mwezi Februari mwaka 2017 baada ya miaka mingi ya kujaribu kumpiku Rais Kabila kwenye chaguzi zilizopita bila mafanikio.

Mwaka huo wa 2017, Rais huyo mteule alichukua uongozi wa chama cha upinzani Union for Democracy and Social Progress (UDPS) kilichoanzishwa na marehemu babake mwaka 1982.

Hata hivyo, alionekana kukata tamaa ya kuwania urais alipojiunga na viongozi wengine wa upinzani Novemba mwaka jana kumuidhinisha Bw Fayulu ingawa chama chake baadaye kilikataa kuidhinisha makubaliano hayo ndipo akawania kiti hicho.