http://www.swahilihub.com/image/view/-/3969834/medRes/1670920/-/tnxe93/-/may.jpg

 

Huenda Theresa May akakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye

Theresa May

Waziri Mkuu wa Uingereza Bi Theresa May. Picha/MAKTABA 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Wednesday, January 16  2019 at  13:57

Kwa Muhtasari

Waziri Mkuu wa Uingereza anakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye.

 

LONDON, Uingereza

BUNGE la Uingereza Jumanne lilifanya kura ya kihistoria kuhusiana na mpango wa Uingereza kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya (EU) uliokubaliwa na umoja huo.

Pande zote za Bunge hilo zinajiandaa kwa kivumbi cha majibizano makali, hasa wakati huu ambapo mpango huo wa Uingereza kujiondoa katika EU umekataliwa.

Chama cha Leba kinataka kura ya kutokuwa na imani na serikali ya May wa chama cha Conservative ifanyike leo Jumatano jioni.

Huku kukiwa kumesalia zaidi ya miezi miwili tu hadi kufikia Machi 29 ambayo ndiyo tarehe iliyowekwa kwa ajili ya kujitoa, Uingereza ambayo imegawanyika kimtazamo pamoja na dunia inasubiri kuona kitakachotokea.

Wachache wanatarajia makubaliano hayo yapite lakini jinsi Waziri Mkuu Theresa May atakavyoshindwa katika kura hiyo ndilo jambo ambalo hasa litaamua iwapo atajaribu tena, ataipoteza nafasi yake kama Waziri Mkuu, atachelewesha kujiondoa kwa Uingereza kutoka kwenye EU au hata iwapo Uingereza itaondoka kwenye umoja huo kabisa.

Wabunge kutoka vyama vyote wanapinga makubaliano hayo kutokana na sababu tofauti lakini hapo juzi May aliwataka wayatazame tena makubaliano hayo.

May alivyonusurika

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May Desemba 13, 2018, alinusurika kura ya kutokuwa na imani naye kutoka kwa wabunge wa chama chake cha Conservative.

Wabunge 200 dhidi ya 117 walipiga kura kumuunga mkono kusalia kuwa kiongozi wa chama hicho na waziri mkuu, lakini hiyo inamaanisha amepoteza uungwaji mkono wa theluthi moja ya wabunge wa chama chake na hivyo kuashiria bado anakabiliwa na changamoto kubwa kutekeleza mpango wake kuhusu mchakato wa Uingereza kujiengua Umoja wa Ulaya.