http://www.swahilihub.com/image/view/-/4054520/medRes/1727099/-/vkqr4b/-/desa.jpg

 

UN yakataa kuunga mkono Raila kususia uchaguzi

Uhuru Kenyatta

Uhuru Kenyatta wa Jubilee (kushoto). Kulia ni Raila Odinga wa muungano wa National Super Alliance (Nasa). Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Thursday, October 5  2017 at  10:07

Kwa Muhtasari

Umoja wa Mataifa (UN) umemtaka kinara wa National Super Alliance (Nasa), Raila Odinga asitishe vitisho vyake kuwa atasusia uchaguzi wa Oktoba 26 na badala yake agombee urais ili Wakenya wawe na mwanya wa kidemokrasia wa kupata uongozi anaoutaka.

 

NEWYORK, Marekani

UMOJA wa Mataifa (UN) umemtaka kinara wa National Super Alliance (Nasa), Raila Odinga asitishe vitisho vyake kuwa atasusia uchaguzi wa Oktoba 26 na badala yake agombee urais ili Wakenya wawe na mwanya wa kidemokrasia wa kupata uongozi anaoutaka.

UN kupitia Mkurugenzi wake katika afisi ya Nairobi, Sahle-Work Zewde imesema kususia uchaguzi sio suala la kutafakariwa bali wote walio katika ushindani
wanafaa kuwa wakijipanga kugombea.

Hilo yumkini ni pigo kubwa kwa Nasa ambapo Odinga amekuwa akitaka UN kuingilia kati na kuhakikisha kuwa matakwa yake ya kupata mabadiliko katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) yametimizwa.

Sahle-Work Zewde ameitaka mirengo ya Jubilee na Nasa badala ya kushida ikitoa makataa kwa IEBC ihakikishe kuwa imeshirikiana na tume hiyo kwa kuwa ndiyo tu imepewa mamlaka ya kikatiba ya kuandaa na kushirikisha uchaguzi nchini Kenya.

Zewde alisema kupitia taarifa ya Jumatano kuwa IEBC imeonekana kuwa inajali uwajibikaji na haki kwa wadau wote kupitia azima yake ya kuandaa mikutano ya kushauriana na mirengo ya ushindani.

UN imesema kuwa ina imani na IEBC - kwamba ina uwezo wa kuwajibikia kura hiyo ya marudio kwa njia ya haki.

Aliutaka mrengo wa Nasa badala ya kuzindua shinikizo “zisizofaa” kwa IEBC, ishiriki mashauriano hayo ya IEBC kwa nia ya kupata mstakabali ufaao ndani ya uwiano.

Zewde pia alivitaka vyama vikuu katika ushindani huo viheshimu uhuru wa idara ya mahakama.

“Ni msimamo wetu kuwa haki za waandamanaji ziheshimiwe na idara za kiusalama bora tu, nao waandamanaji wachunge kujiingiza katika visa vya kuvunja haki za wengine,” amesema Zewde.

Amesema kuwa ni haki pia ya wasioshiriki katika maandamano hayo walindwe kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya kutoa taarifa hiyo, Zewde alikuwa amekutana na IEBC, huku nayo tume hiyo ikiwa imeandaa mkutano wawakilishi wa Nasa na wale wa Jubilee.