http://www.swahilihub.com/image/view/-/2837684/medRes/1095354/-/137kdg1/-/578861-01-02%25282%2529.jpg

 

Mapasta walioshukiwa kupeleleza wazuiwa kuondoka

Muhanad Mustafa

Wakili Muhanad Mustafa anayetetea mapasta wawili wa Sudan Kusini walioachiliwa huru na mahakama Agosti 5, 2015 ambapo walikuwa mametuhumiwa na kosa la upelelezi. Picha/AFP 

Na AFP

Imepakiwa - Tuesday, August 18  2015 at  15:53

Kwa Muhtasari

Mapasta wawili raia wa Sudan Kusini walioachiliwa huru na mahakama ya Sudan wiki mbili zilizopita, bado wamezuiliwa kuondoka nchini humo.

 

KHARTOUM, Sudan

MAPASTA wawili raia wa Sudan Kusini walioachiliwa huru na mahakama ya Sudan wiki mbili zilizopita, bado wamezuiliwa kuondoka nchini humo.

Mapasta hao, Yat Michael, 49 na Peter Yen, 37 waliachiliwa huru wiki iliyopita baada ya mahakama kutowapata na hatia ya kuwa majasusi wa serikali ya Sudan Kusini.

Rebecca Antony, mkewe Yat Michael, aliambia wanahabari kuwa familia yake imezuiliwa kusafiri nje ya nchi ya Sudan bila kupewa sababu yoyote.

'’Mimi, mume wangu pamoja na mtoto wetu tulijaribu kusafiri nje ya nchi tukazuiliwa na maafisa wa usalama bila kupewa sababu yoyote au kuonyeshwa stakabadhi za agizo la mahakama,’’ akasema.

'’Hatujui kwamba serikali inataka nini kutoka kwetu hata baada ya kuachilia huru mume wangu mnamo Agosti 5 ’’ akaongezea.

Muhanad Mustafa, kiongozi wa mawakili waliokuwa wakitetea mapasta hao mahakamani Jumanne alikashfu vikali hatua ya serikali kuzuia wateja wao kusafiri nje ya nchi.

Mustafa alishutumu Idara ya Upelelezi pamoja na Idara ya Kijasusi kwa kuzuilia wawili hao kusafiri nje ya nchi kuelekea Sudan Kusini. Alisema kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria.

“Ni kinyume cha sheria kuwazuilia mapasta wawili kusafiri nje ya nchi bila kuwapa sababu,” akasema.

'’Tutaelekea mahakamani ili ishinikize serikali kutii uamuzi wake kwa kuwaruhusu mapasta hao kusafiri nje ya nchi bila kuwekewa vizuizi na maafisa wa usalama,” akaongezea.

Hata hivyo, serikali ya Sudan haijatoa taarifa kuhusiana na madai hayo.

Mahakama ya Khartoum ilitupilia mbali mashtaka manne, likiwemo shtaka la kuendesha shughuli za kijasusi, dhidi ya mapasta hao na kuagiza waachiliwe huru.

Kutishia mfumo wa Katiba

Mashtaka mengine yalikuwa kutishia mfumo wa katiba ya Sudan, kutishia usalama, kujipatia taarifa za siri za serikali na kuzua chuki miongoni mwa madhehebu mbalimbali ya kidini.

Maafisa wa usalama wa Sudan wamekuwa na mazoea ya kuvamia makanisa mara kwa mara kutokana na sababu zisizojulikana.

Asilimia kubwa ya raia wa Sudan ni Waislamu. Sudan imeorodheshwa ya sita kati ya mataifa 50 duniani ambapo Wakristo wako katika hatari kubwa ya kuteswa.

Mwaka uliopita, kesi dhidi ya Meriam Yahia Ibrahim ilizua mjadala mkali ulimwenguni baada ya mahakama ya Sudan kumhukumu adhabu ya kifo.

Meriam alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kubadilisha Imani yake kutoka Uislamu na kuwa Mkristo na pia kuoana na mwaume Mkristo ambaye ni wa asili ya Sudan Kusini-Amerika.

Meriam alitoroka Sudan mnamo Julai 2014 kufuatia makabiliano makali mahakamani.