http://www.swahilihub.com/image/view/-/2900756/medRes/1139289/-/iw1uvcz/-/851746-01-02.jpg

 

Mashambulizi nchini Syria yatamtesa Assad?

Bashar al-Assad

Rais wa Syria Bashar al-Assad kwenye mahojiano katika kituo cha runinga; mahojiano yakipeperushwa na Khabar TV Oktoba 4, 2015. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  11:48

Kwa Muhtasari

Mashambulizi nchini Syria yatamtesa Assad?

 

DOUMA, Syria

NI swali gumu ambalo halina majibu kwa muda huu baada ya Syria kushambuliwa mfululizo usiku wa kuamkia Jumamosi na muungano wa wanajeshi wa Uingereza, Marekani na Ufaransa.

Shambulio hilo nchini humo lilifanyika baada ya Syria kudaiwa kurusha kemikali za sumu katika eneo lililo chini ya waasi katika mji  wa Khan Sheikhoun; ilipo ngome yao nchini humo.

Nchi hizo tatu zilifanya mashambulizi mengi zaidi juzi kuliko mwaka  mmoja uliopita.

Hata hivyo, maofisa wa ngazi za juu wa Marekani hawana uhakika kama mashambulizi hayo yatafanikisha lengo la kuuzuia utawala wa Rais Bashar al-Assad kutumia tena silaha za sumu.

Utawala wa Trump uliweka  wazi kwamba, mashambulizi dhidi  ya mpango wa silaha za sumu wa  Syria yalikuwa na lengo la kumzuia Rais Assad kutumia tena silaha kama hizo.

Rais wa Marekani, Donald  Trump  aliahidi  hatua  za haraka  na  kali  za  kijeshi akimshutumu Assad na kuzikejeli nchi za Urusi na Iran kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Maandishi hayo ya Twitter yalizusha taharuku kimataifa juu  ya shambulio ambalo litatokea katika moja kati ya maeneo yenye  matatizo na kuwaacha maofisa wa Marekani wakijaribu kutafuta  majibu.

Wakati shambulio hilo likitokea siku kadhaa baada ya Trump kutoa muda wa awali, kulikuwa na washirika wawili na mtazamo wa kupunguza malengo ya mashambulizi hayo ulikuwapo. Kwa wachunguzi wengi wa masuala ya kivita hatua za kijeshi zilionekana zaidi kama jibu lililowekewa  mipaka kuliko shambulio kubwa  ambalo lilielezwa  hapo kabla.

Hali hiyo imesababisha maswali kadhaa kubwa ikiwa ni je, Assad atakuwa amepata hofu na kujizuia kutumia silaha za sumu?

“Sina shauku,” anasema Ryan Crocker, balozi wa zamani wa Marekani  nchini  Syria ambaye  pia  alifanya kazi kama mjumbe  wa Marekani  nchini  Irak, Afghanistan  na  Pakistan.

“Tulifanya  kitu kama  hicho mwaka mmoja  uliopita  katika  kiwango  kidogo, lakini mashambulizi haya hayatafanya  uharibifu  wa  kudumu  kwa  uwezo wa  Assad wa  kuzitumia silaha  za sumu hapo baadaye  ama kitu kingine zaidi”.

“Hilo ni swali  ambalo  linabaki wazi,”  anasema  Philip Breedlove, kamanda wa  zamani  wa  NATO  na  jeshi  la  Marekani  barani Ulaya.

“Kumbuka kwamba mhalifu huyu, kiongozi huyu ‘zimwi’ wa Syria anapata uungwaji mkono na  uwezo wa  kisiasa  kutoka Urusi na Iran.”

Wakati ni vigumu  kutabiri jibu la Assad, kubadili utaratibu wake utahitaji  hatua  ambazo  zinatishia  msingi  halisi wa  utawala wake, amesema Mona Yacoubian, msomi raia wa Syria katika taasisi ya amani ya Marekani.

Katika hali  hiyo, mashambulizi  hayo huenda ni madogo kuweza kutimiza lengo lililokusudiwa.

Viongozi  wa  mataifa ya Kiarabu, akikosekana Rais wa  Syria  walikutana Saudi Arabia kwa ajili ya  mkutano uliofanyika jana wakati mataifa yenye nguvu duniani  yakipambana kuhusu Syria na  hali ya wasiwasi ikiongezeka kati ya Saudi Arabia na Iran.

Saudi Arabia inataka uwepo msimamo mkali na wa pamoja dhidi  ya  hasimu  wake  mkubwa  Iran  katika  mkutano  huo  wa  kila mwaka wa mataifa 22  wanachama  wa Jumuiya  ya  Nchi za Kiarabu (Arab league). Mataifa  hayo  makubwa katika  eneo  la  Mashariki  ya Kati yanapigana vita nchini  Syria na katika eneo la Kusini  mwa Saudi Arabia katika  nchi  jirani  ya  Yemen, yakiunga mkono pande  zinazopingana nchini Irak na Lebanon

Wakati vuguvugu hilo la mashambulizi likiendelea, kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei amewashutumu Rais Trump na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron akisema shambulio lililofanywa na nchi hizo dhidi ya Syria ni uhalifu.

‘‘Rais wa Marekani, Rais wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Uingereza ni wahalifu,” alisema Khamenei.

Urusi imeuomba Umoja wa Mataifa (UN) uitishe kikao cha dharura cha Baraza la Usalama kujadili shambulio hilo ambalo limedai linahatarisha usalama wa wananchi wa Syria.

Trump alisema awali kwamba, alitoa amri vikosi vya nchi yake kushambulia maeneo yanayohusiana na silaha za kemikali zinazomilikiwa na utawala wa al-Assad.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alisema kwamba mashambulizi ya Marekani, Uingereza na Ufaransa dhidi ya Syria yalikuwa majibu ya ‘lazima na mwafaka’ kuelekea maeneo yanayohisiwa kutumia silaha za kemikali katika mji wa Douma.

 

Wanasiasa Urusi, Assad wakutana

Ziara ya wanasiasa hao imefanywa ikiwa ni siku moja baada kuripotiwa  kuwa wakaguzi kutoka Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Matumizi ya Silaha za Sumu – OPCW wanatarajiwa kuanza uchunguzi wao wa kubaini kama silaha za gesi ya klorini au sarin zilitumiwa dhidi ya raia katika shambulizi  la Aprili 7, 2018, mjini Douma.