http://www.swahilihub.com/image/view/-/3452196/medRes/1487880/-/byxtupz/-/neda.jpg

 

Mbunge wa EALA atetea Rais John Magufuli

Bi Mumbi Ngaru

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bi Mumbi Ngaru akiwa uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) Oktoba 6, 2014. Picha/EVANS HABIL 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, November 14  2017 at  16:41

Kwa Muhtasari

Mwanasiasa wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kutoka Mlima Kenya, Mumbi Ng’aru amekejeli Wakenya kwa kuona taifa la Tanzania kuwa adui wa ushirika katika jumuia ya Afrika Mashariki.

 

MWANASIASA wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kutoka Mlima Kenya, Mumbi Ng’aru amekejeli Wakenya kwa kuona taifa la Tanzania kuwa adui wa ushirika katika jumuia ya Afrika Mashariki.

Alimtetea rais John Pombe Magufuli wa Tanzania akimtaja kama mmoja wa wachache Afrika ambao wanaelewa wanachokifanya mamlakani na aliye na uwezo wa kuwa mwalimu wa Kenya kuhusu utawala wa kujali masilahi ya wanyonge.

Bi Ng’aru ambaye kwa sasa ndiye aliyevuna nafuu zaidi eneo la Mlima Kenya kwa kujihusisha na ODM kwa kuwa ameteuliwa kuwa mbunge katika bunge la Afrika Mashariki (EALA) akiwa Mjini Thika alisema, “Wakenya tulieni mpewe somo la utawala bora na Tanzania.”

Alisema kuwa tofauti ya utawala wa Kenya na Tanzania ni kuwa ule wa hapa hutilia mkazo zaidi haki za mabwanyenye huku za mnyonge zikikandamizwa.

“Katika taifa la Tanzania, hakuna haki za mnyonge zikiwa zimeorodheshwa kama za Mutumba na hakuna haki za hadhi ambazo hutengewa mabwanyenye. Wote Tanzania ni sawa huku nchini Kenya wengine wakiwekwa katika kiwango cha kuwa sawa kuwaliko wenzao,” akasema.

Alisema kuwa mifugo wa Kenya wakirandaranda na kuingia katika taifa la Tanzania, basi serikali ya Tanzania iko na uhalali wa kuitwaa ili mipaka ya ujirani iheshimiwe kati ya mataifa yoyote yale.

Amesema kuwa Wakenya wanaona kama ni ugaidi kwa serikali ya Tanzania kunasa na kuchoma vifaranga ambavyo vilikuwa vikiingizwa katika taifa hilo kimagendo na Wakenya.

“Ikiwa magendo hapa Kenya ni ya kukubalika, komeni kuifanya Tanzania iwe mshirika wa kushurutishwa. Ikiwa Tanzania imekataa kuiga magendo yenu na kuyakumbatia kama sera inafaa uelewe ni haki yao na rais wao,” akasema.

Amesema kuwa hapa Kenya mifugo wa mabwanyenye hulishwa katika mashamba ya wanyonge ambapo mimea huharibiwa na kuwatwika njaa wanyonge hao, huku serikali ikionekana kutojali hali hiyo.

Ng’aru amesema kuwa tofauti kuu kati ya Kenya na Tanzania kiutawala ni kuwa wetu (Kenya) ni utawala wa kuviziana na kuangamizana kiuchumi, kisiasa na kijamii huku Tanzania ikiwa ni sawa na ngome ya usawa na uhalali wa kutekeleza masuala ya kiuongozi.