http://www.swahilihub.com/image/view/-/4937330/medRes/2225494/-/v9jgrp/-/mavifoki.jpg

 

Rais Kenyatta: Operesheni imekamilika eneo la shambulizi Riverside

Ambulensi

Ambulensi zikiwa zimeegeshwa eneo la shambulizi la kigaidi, 14 Riverside Drive Complex, Nairobi mapema Jumatano, Januari 16, 2019, siku moja baada ya shambulio. Picha/DENNIS ONSONGO 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, January 16  2019 at  11:26

Kwa Muhtasari

Rais Uhuru Kenyatta amesema magaidi waliotekeleza shambulizi katika jumba lenye biashara kadhaa ikiwemo ile ya hoteli ya DusitD2 wameuawa.

 

WATU 14 ndio wamepoteza maisha yao kufuatia shambulizi la kigaidi lililofanyika jana katika jumba la kibiashara la 14 Riverside Drive mtaani Westlands jijini Nairobi.

Kwenye salamu zake za kufariji taifa mapema Jumatano Rais Uhuru Kenyatta hata hivyo, amesema operesheni ya kuokoa manusura na hata jengo lenyewe imekamilika.

Aidha, Rais Kenyatta amethibitisha kwamba magaidi wote wameuawa.

Kulingana na kanda za kamera za siri, wanaume wanne walionekana wakiingia katika jengo hilo, wawili wakafanya majaribio ya bunduki kwa kufyatua risasi kabla ya kuanza mashambulizi.

Kulingana na manusura walioongea na vyombo vya habari, magaidi hao walifyatua risasi kwa kila waliyeona.

"Kufikia leo Jumatano asubuhi, zaidi ya watu 700 wameokolewa kutoka jengo hilo na maafisa wetu jasiri wa usalama," amesema kiongozi wa nchi akihutubu katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi.

Riverside Drive ni jumba lenye maduka, ofisi, benki, hoteli ikiwamo Dusit D2 ambayo iliathirika zaidi kwa shambulizi hilo.

Mkasa huo ulitukia kuanzia Jumanne saa tisa za mchana, ambapo vikosi vya pamoja vya maafisa wa usalama vimechukua zaidi ya saa 12 kukabiliana na magaidi hao wanaoshukiwa kuhusishwa na kundi haramu la al-Shabaab.

Milio ya risasi

Ufyatulianaji wa risasi na vilipuzi uliskika wakati huo na alfajiri Jumatano.

Kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta amesema waliopata majeraha ya risasi wametibiwa na wengine kuendelea kuhudumiwa. Mbali na kutibiwa, walioathirika pia wanapata ushauri nasaha.

Majeruhi walipelekwa katika hospitali mbalimbali jijini Nairobi, ikiwamo ya Rufaa ya Keyatta, KNH, MP Shah, na Avenue Hospital.

Rais Kenyatta ambaye ametaja magaidi hao kama 'genge la wahalifu' linalolenga kuhangaisha wananchi, amesema serikali haitasita kupambana vilivyo na magaidi nchini.

Ameshukuru maafisa wa usalama waliojitokeza kijasiri pamoja na Wakenya waliosimama kidete kufariji wenzao kupitia mitandao na kutoa damu kwa majeruhi.

"Maafisa wetu na wananchi wameonesha ujasiri, uzalendo na wasiotikishwa na magaidi kupitia ushirikiana wao katika mkasa huo," akasema, akisisitiza kuwa usalama umeimarisha na taifa hili ni salama. Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuimarisha utendakazi wa asasi za usalama.

Kwenye taarifa yake, Kenyatta ametangaza kuwa waliopanga na kufadhili shambulizi hilo watakabiliwa vilivyo na mkono wa sheria.

Akitoa salamu zake za pole, Rais alikuwa ameandamana na Naibu wake Dkt William Ruto, mawaziri Dkt Fred Matiang'i (Usalama wa Ndani), Raychele Omamo (Ulinzi), Mkuu wa Majeshi nchini Samson Mwathethe, na viongozi wengine wanachama wa baraza la kitaifa la usalama.

Dkt Matiang'i na Inspekta Mkuu wa Polisi (IG) Joseph Boinnet ndio walijukumika kutoa taarifa kwa taifa mnamo Jumanne kuhusu hatua waliyopiga maafisa wa usalama kukabiliana na shambulizi na kukomboa jumba la Riverside Drive.